0

Yondani, Abdul wana tuzo yao

Yondani, Abdul wana tuzo yao

Sat, 8 Aug 2020 Source: Mwanaspoti

MABOSI wa Yanga ni kama wamejishtukia na pengine kutokana na kelele za mashabiki juu ya nyota wao wakongwe Kelvin Yondani, Juma Abdul na Mrisho Ngassa walioamua kuwamwaga, sasa wamesema wamepanga kuwapa tuzo ya heshima kwenye kilele cha Siku ya Mwananchi.

Kilele cha siku hiyo kitafanyika mwishoni mwa mwezi huu kikitumika kwa Yanga kutambulisha nyota wake wapya sambamba na jezi mpya kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, huku uzinduzi wake ukipangwa kufanyika Jumamosi ijayo mjini Dodoma.

Habari kutoka ndani ya Yanga, mabosi wa klabu hiyo wameona ni vyema kuwapa heshima wachezaji hao siku ya kilele hicho, licha ya kwamba baadhi yao wanaendelea kuzungumza nao kuwapa mkataba mpya wa kuitumikia timu hiyo.

Mmoja wa viongozi wa Yanga alisema bado wapo katika mazungumzo na Yondani waliyempa ofa yao ambaye aliomba kwenda kutafakari na wanapenda kuendelea naye kutokana na heshima aliyojiwekea katika timu hiyo.

“Yondani tulimueleza hali halisi kwamba hakutokuwa na pesa ya usajili, lakini kwenye upande wa mshahara wake kuna ongezeko kubwa, lengo ni kwamba tuachane naye kwa heshima na tunathamini alichokifanya,” alisema kiongozi huyo aliyekataa kutajwa jina lake gazetini na kuongeza;

“Kama atapata timu nyingine hatuwezi kumzuia kwenda huko, ila Siku ya Wananchi tutamuomba aje kwani, yeye, Juma Abdul na Mrisho Ngassa wana heshima katika klabu yetu hivyo kuna zawadi ambayo wataandaliwa.”

Chanzo: Mwanaspoti

Join our Newsletter