0

Morocco awasifu wachezaji wake  

Morocco awasifu wachezaji wake  

Tue, 23 Feb 2021 Source: HabariLeo

KOCHA wa Namungo FC, Hemed Morocco amesema licha ya kikosi chake kuibuka na ushindi mnono, wachezaji wake walifanya makosa anayotakiwa kuyafanyia kazi kujipanga na mchezo wa marudiano unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam keshokutwa.

Juzi, Namungo iliibuka na ushindi wa mabao 6-2 dhidi Primeiro de Agosto ya Angola katika mchezo wa ugenini uliochezwa Uwanja wa Azam, matokeo yaliyowaweka kwenye nafasi nzuri ya kuangika rekodi mpya kutinga hatua ya makundi.

Akitoa tathimini baada ya kukamilika kwa mchezo huo, Morocco aliwapongeza wachezaji wake na kuwataka wasifurahie kwani bado wana kazi kubwa ya kufanya mbele yao.

“Nawapongeza wachezaji wamefanya kazi nzuri, lakini hatutakiwi kufurahia kwani bado tuna kazi kwenye mchezo wa marejeano ambao tunahitaji kujipanga upya,” alisema.

Morocco alisema mechi hiyo ilikuwa nzuri ingawa walianza kucheza kwa kusuasua lakini kadri muda ulivyosonga mbele wachezaji wake walianza kuzoea na kuanza kutawala mchezo.

“Mchezo ulikuwa mzuri ingawa tulianza kwa wasiwasi na baadae tukaanza kutawala mchezo, wapinzani wetu walikuwa wazuri na wachezaji wangu hawapaswi kufurahia ushindi tuliopata.”

“Tunahitaji kujipanga kwa mchezo ujao ambao kwanza kufanyia kazi makosa waliyofanya wachezaji wangu ndiyo maana tumeruhusu kufungwa mabao mawili,” alisema.

Alisema lengo lao ni kujipanga kuhakikisha mchezo wa marejeano wanafanya vizuri zaidi ili kuhakikisha wanatinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Chanzo: HabariLeo