0

Makundi Ligi ya Mabingwa wa Mikoa kuanza Machi 4

Thu, 25 Feb 2021 Source: habarileo.co.tz

HATUA ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) inatarajia kuanza Machi 4 katika vituo vinne vyenye timu saba kila kimoja.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo alisema vituo vitakuwa Arusha, Pwani, Lindi na Katavi.

“Vituo vitakuwa katika mikoa ya Arusha, Pwani, Lindi na Katavi na kila kituo kitakuwa na timu saba ambazo zitachuana katika hatua za awali na baadaye timu mbili katika kila kundi zitafuzu kucheza fainali,” alisema Ndimbo.

Kituo cha Arusha kitakuwa na timu za Kundi A ambazo ni wenyeji TMA Stars, Sinai Rangers (Manyara), Sharp Strickers (Tanga), TRA (Kilimanjaro), Mara Sports Academy (Mara), Copco Veteran (Mwanza) na Huduma FC (Dar es Salaam).

Kundi B kituo cha Pwani kuna wenyeji Baga Friends, Temeke Squad (Dar es Salaam), 515 KJ (Morogoro), Manyoni Sports Center (Singida), Kimara United (Dodoma), Annuary FC (Shinyanga) na Bariadi United (Simiyu).

Kundi C kituo cha Lindi kuna wenyeji Lindi United, Mkuti Market (Mtwara), Mabomba FC (Dar es Salaam), Top Boys FC (Ruvuma), Njombe Academy (Njombe), Mtwivila FC (Iringa) na Itezi FC (Mbeya).

Kituo cha Katavi cha Kundi D kitakuwa na wenyeji timu ya Tanesco FC, Sumbawanga United (Rukwa), Mapinduzi FC (Songwe), Black Stars (Tabora), Toto Kigoma FC (Kigoma), Nyaishozi FC (Kagera) na Nyakumbu FC (Geita).

Waamuzi wa kati 42 na waamuzi wasaidizi 59 wameitwa kwenye semina inayotarajiwa kuanza kesho kwa ajili ya mchujo kupata waamuzi watakaokwenda kuchezesha mechi hizo.

Chanzo: habarileo.co.tz