0

Kibabe tu!, cheki Namungo ilivyotoboa Caf

Kibabe tu!, cheki Namungo ilivyotoboa Caf

Thu, 25 Feb 2021 Source: Mwanaspoti

By Olipa AssaMore by this Author SAFARI ya Namungo katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ilianza kama utani, lakini vijana hao wa Ruangwa wako siriaz ile mbaya na tayari wameingiza mguu mmoja kwenye hatua ya makundi.

Haikuwa safari nyepesi kwa Namungo kufikia hatua hiyo, imekutana na changamoto za hapa na pale ikiwamo kushindwa kucheza dhidi ya CD Primeiro de Agosto nchini Angola, baada ya kutolewa taarifa na wenyeji wao kwamba wachezaji Fredy Tangalo, Lucas Kikoti, Hamis Mgunya na mtendaji mkuu Omary Kaaya, wana virusi vya corona, hivyo kutakiwa timu nzima ikae karantini.

Jambo hilo liligomewa na viongozi wa Namungo ambao iliwalazimu kubaki garini, hali iliyosababisha mchezo huo kufutwa kabla ya Kamati ya Caf kuamua mechi zote mbili zichezewe Tanzania.

Katibu wa timu hiyo, Ally Suleiman aligusia baadhi ya changamoto ambazo walikutana nazo Angola kuwa ni kulala na njaa, kukaa garini kwa muda mrefu na hatimaye haki ikapatikana katika mechi yao ya kwanza iliyopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kwa De Agosto ambao walikuwa wenyeji wa mchezo kuchapwa mabao 6-2.

Namungo inashiriki kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo na imeonyesha uwezo wa kufika hatua nzuri na inahitaji japo sare au kipigo kisichozidi tofauti ya mabao manne ili kuingia hatua ya makundi.

Wakati michuano hiyo inaanza viongozi wa Namungo kupitia kwa Katibu Suleiman, walikaririwa na Mwanaspoti kwamba bajeti yao ilikuwa Milioni 500, ingawa hawakuwa na uhakika wa kufika hatua waliyopo sasa ya mwisho ya mchujo.

Chanzo: Mwanaspoti