0

Azam FC yaivulia kofia Prisons

Azam FC yaivulia kofia Prisons

Thu, 25 Feb 2021 Source: HabariLeo

WANALAMBALAMBA wa Chamazi, Azam FC wamewavulia kofia Tanzania Prisons baada ya kushindwa kuwafunga katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakisema ulikuwa mchezo mgumu na wenye matumizi ya nguvu.

Timu hizo zilishindwa kufungana katika mchezo huo uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex baada ya kucheza dakika 90 na kutoka suluhu.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati alisema timu zote zilicheza vizuri na wapinzani wao walikuwa vizuri na wenye nguvu kiasi cha kufanya mchezo huo kuwa mgumu.

“Ulikuwa ni mchezo wenye nguvu kubwa, timu zote zilikuwa kwenye kasi mwanzo hadi mwisho, tulitengeneza nafasi za kufunga tulishindwa kuzitumia kwasababu wapinzani wetu walikuwa makini katika lango lao,” alisema.

Alisema matokeo hayo hayawezi kuwakatisha tamaa juhudi zao za mapambano bali wanajipanga na kufanya maboresho ili kufanya vizuri zaidi katika michezo ijayo.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC iliyocheza mechi 21 kufikisha pointi 37 ikiwa nafasi ya tatu na Prisons ipo nafasi ya nane na pointi zake ni 26 ikiwa imecheza mechi 20.

Kabla ya kucheza mchezo mwingine wa ligi, timu hiyo inajiandaa kuikabili Mbuni FC katika mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho la Azam (FA) utakaochezwa Jumamosi hii.

Chanzo: HabariLeo