0
MenuInfos
Dini

AUWSA yazijengea shule 19 vyoo bora

AUWSA yazijengea shule 19 vyoo bora

Thu, 25 Feb 2021 Source: HabariLeo

MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira ya Jiji la Arusha (AUWSA) imejenga vyoo vya mfano katika shule 19 za sekondari na msingi jijini Arusha ili kuwapa mazingira salama kwa afya wanafunzi wa kike.

Aidha, wakuu wa shule hizo wamesisitizwa kusimamia usafi wa vyoo na kuhakikisha watoto hawaharibu miundombinu yake ili vidumu kwa muda mrefu.

Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, James Lebikoki alisema jana katika makabidhiano ya vyoo hivyo kuwa, walimu wakuu na wakuu wa shule husika wanapaswa kuhakikisha vinatumika ipasavyo, vinahudumiwa na kutunzwa ili vidumu zaidi.

"Inashangaza kuona baadhi ya vyoo vipya vya mfano na bora, ambavyo serikali imetumia gharama kubwa kuvijenga, eti koki zimeng'olewa na walimu wapo wanaangalia tu," alisema.

Alishauri wakuu hao kuwabana wafanyabiashara katika maeneo ya shule wakiwamo wanaouza mihogo, karanga na vitu vingine shuleni, kufanya usafi wa mazingira wanayofanyia biashara zao wanapomaliza shughuli zao.

Mhandisi Mshauri, Praygod Mawalla, alisema mradi wa ujenzi wa miundombinu ya afya na usafi wa mazingira, unatekelezwa na AUWSA kupitia BQ Contractors, Caberisa Company Limited na Shreeji Construction Company Ltd.

Alisema mradi huo umetumia mafundi wanaopatikana katika maeneo ya mradi huo ili jamii husika zinufaike kwa kuinuka kiuchumi.

"Lengo la ujenzi wa vyoo hivi vya mfano katika maeneo ya mradi, ni kusaidia hata kubadilisha hata jamii zinazowazunguka kutoa kipaumbele katika ujenzi wa vyoo bora na klabu za afya, maji na usafi wa mazingira (AMAU), zilizoundwa kwenye shule hizi, zitasaidia kuleta mabadiliko katika shule na jamii zao," alisema.

Alitaja shule zilizojengwa vyoo hivyo vya mfano kuwa ni sekondari mbili za Kinana na Mrisho Gambo.

Mhandisi Mawalla alizitaja shule za msingi 17 kuwa ni Mateves, Unga Ltd, Sokoni 1, Elerai, Terat, Engasengiu, Sinoni, Ukombozi, Kijenge, Muriet, Darajani, Daraja 2, Maweni, Sombetini, Olasiti, Osunyai, Magereza na Mwangaza.

Alisema kupitia mradi huo, piawamejenga vyoo bora katika Kituo cha Afya cha Moivo na Zahanati ya Mateves, masoko ya Oldonyokumri na Mbauda, Uwanja wa Michezo Gymkhana na Ofisi ya Kata ya Moivaro.

Awali, Ofisa Elimu wa Jiji la Arusha, Omar Kwesiga, alipongeza ujenzi huo wa vyoo bora na vya mfano, akiahidi kutoa maelekezo ya kwa shule kuhusu uwepo wa klabu zitakazosaidia usafi wa mazingira na vyoo hivyo.

Chanzo: HabariLeo