0
MenuInfos
Afya

Vijana 42 wapewa kadi bima ya afya

Fri, 26 Feb 2021 Source: habarileo.co.tz

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Mussa Mkombati, ametoa kadi za bima ya afya kwa vijana zenye thamani ya Sh milioni 1.2 huku akihimiza wananchi kuona umuhimu wa kujiunga na mfuko huo ili kuwa na uhakika wa matibabu.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi kadi hizo za Bima wa Afya ya Jamii Iliyoboreshwa (CHIF) kwa vijana 42, alisema wananchi wanapaswa kujiwekea uhakika wa matibabu kwa kuwa na kadi za bima.

Alisema ameamua kutoa kadi hizo kwa vijana kwa kuwa ndio nguvu kazi kubwa ya uzalishaji, hivyo lazima wawezeshwe kuwa na uhakika wa matibabu.

"Tunamshukuru Rais John Magufuli kwa kuwajali wanyonge kwani kwa gharama ndogo ya Sh 30,000, kaya yenye watu sita ina uhakika wa kupata huduma za matibabu mwaka mzima bila usumbufu," alisema.

Vijana walionufaika na msaada huo walisema hatua hiyo ni muhimu kwao kwani sasa wataweza kulinda mitaji yao, badala ya kulazimika kuitumia kwa matibabu.

Mmoja wa vijana hao, Hussein Musa alisema sasa watafanya shughuli za uzalishaji bila ya hofu kwani kadi hizo zitawasaidia kupata huduma bila ya kutumia gharama za ziada.

Azimina Mhando, alisema kadi hizo zitakuwa mkombozi kwani zitawaepusha kutumia gharama kubwa za matibabu kutokana na maboresho makubwa ya huduma za afya yaliyofanywa na serikali.

Chanzo: habarileo.co.tz