0
MenuInfos
Afya

Mpango: Mungu kanitendea miujiza

Mpango: Mungu kanitendea miujiza

Thu, 25 Feb 2021 Source: HabariLeo

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema Mungu amemtendea miujiza baada ya kupona na kutoka hospitalini.

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Aisema aliiugua kwa siku 14 kwa kubanwa kifua, tatizo ambalo alikuwa analipata tangu utoto wake na alikwenda hospitalini hapo na mtungi wa gesi.

Mbunge huyo wa Buhigwe mkoani Kigoma, alisema sasa ameanza kufanya kazi ndogo ndogo ikiwa ni pamoja na kusaini hundi za mishahara kwa watumishi.

“Mungu aliyetuumba sote amenitendea makuu...tangu wakati naumwa nyumbani hadi hapa hospitalini, mwacheni Mungu aitwe Mungu. Tuendelee kumtukuza. Kwa huruma yake amenipa nafasi tena kuwatumikia Watanzania,” alisema Dk Mpango.

Aliwakumbuka wote waliotangulia mbele ya haki wakati akiwa hospitani akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, mwalimu wake Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mstaafu, Profesa Benno Ndulu na Mbunge wa Kibondo, Atashasta Nditiye.

Alisema amepona na kwa siku tatu hajawekewa mtungi wa gesi na sasa anarejea kazini kuendelea kusimamia mapato na matumizi ya serikali, mikopo na misaadaa na kulinda na kusimamia nidhamu katika matumizi ya serikali.

“Nimepona na kazi ndogo ndogo nimeanza mfano kudhinisha mishahara na wale wenye akaunti NMB nadhani wameona kitu kwenye akaunti zao,” alisema Dk Mpango.

Aliwapongeza madaktari, waganga na wahudumu wote kwa kujitolea na kumsaidia kwa moyo na aliwaombea kwa Mungu wagonjwa waliobaki hospitalini kama alivyomponya yeye atawaponya.

Alimshukuru Rais John Magufuli na familia yake, watendaji wa ofisi kwa kumpigia simu mara mbili au tatu kwa siku kumjulia hali.

Alimshukuru Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma na viongozi wengine pamoja na Watanzania kwa kumuombea na sasa ametoka salama.

Aliwashukuru Watanzania na viongozi wa dini kwa kumuombea na ameona maajabu pamoja na wapigakura wa Jimbo la Buhigwe ambao walipata shida kutokana na uvumi wa kwenye mitandao kwamba amekufa sasa wajue amepona na atafika kuwaona.

Alisisitiza Watanzania kupenda chao kwani alishawishiwa aende hospitali nyingine akasema anaendelea kupata tiba Benjamin Mkapa ambako amepata huduma bora ya kisasa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu, Dk Alphonce Chandika, jopo la madaktari waliokuwa wakimtibu wakiongozwa Dk Antony Yunda na wauguzi wote pamoja na wahudumu kwani alikuwa na wakati mugumu hao ni ndugu zake.

Aliahidi kwenda kumshawishi Rais Magufuli kuipa kipaumbele sekta ya afya ili kuongeza bajeti ya kutosha, kuongeza uwekezaji na kusaidia kuondoa changamoto za watendaji wa hospitali hiyo na nyingine za Makao Makuu ya Serikali jijini Dodoma.

Akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Chandika aliwataka Watanzania kuvipenda vya kwao, ambapo zamani walikwenda kutibiwa India na Uingereza, lakini sasa wanaweza kutibiwa nchini kutokana na huduma kuimarika katika hospitali hiyo.

Chanzo: HabariLeo