0

Snura aelezea alivyovishwa kofia na Rais Magufuli

9a64f0ad90b940f784ebe495fe4980fd Snura aelezea alivyovishwa kofia na Rais Magufuli

Thu, 8 Oct 2020 Source: habarileo.co.tz

MSANII wa muziki wa Bongo Fleva na muigizaji, Snura Mushi amesema kutumbuiza vyema jukwaani ndiko kulikomshawishi Rais John Magufuli kumvalisha kofia.

Snura alivalishwa kofia hiyo na Rais Magufuli Septemba 21 katika Jimbo la Urambo, mkoani Tabora, kwenye kampeni za kuomba kura kwa wananchi za mgombea huyo wa urais kupitia CCM ili aweze kuchaguliwa tena kwa kipindi cha miaka mitano mingine.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Snura ambaye ni msanii wa kwanza wa kike kuvalishwa kofia na Rais Magufuli, alisema Mungu ndiye alipanga kwani alishapita na mgombea huyo kwenye mikoa kadhaa ikiwamo Kagera lakini hakupata fursa hiyo.

“Kufanya kazi bora ya kutumbuiza jukwaani nadhani ilimshawishi Rais kunivalisha kofia na kuwa mwanamke wa kwanza baada ya kufanya hivyo kwa wasanii wengi wa kiume wakiwamo Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Ali Kiba.

“Wakati naimba jukwaani sikujua kuna tukio litatokea, baada ya kumaliza kuna mtu alinipa ishara ya kwenda jukwaa kuu ndipo Rais akanivalisha kofia,” alisema.

Snura amewahi kutamba na vibao kadhaa ikiwamo ‘Majanga’ kilichotoka mwaka 2013.

Chanzo: habarileo.co.tz