0

‘Sheria ya hakimiliki hainufaishi walengwa’

Thu, 8 Oct 2020 Source: habarileo.co.tz

IMEELEZWA kuwa utekelezaji wa Sheria ya Hakimiliki na Shirikishi ya Mwaka 1999 nchini siyo wa kuridhisha katika kuhakikisha waandishi, wavumbuzi na wasanii wananufaika na kufurahia matunda ya kazi zao.

Hayo yalijitokeza katika siku ya nne ya warsha kuhusu uandishi wa kitaaluma inayofanyika katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) jijini Dar es Salaam ambapo washiriki wameelezea madhara ya kutotekelezeka kwa sheria hiyo, kitu ambacho kinachangia kudumaza upatikanaji wa haki za wasanii katika fani mbalimbali.

Profesa Mugyabuso Mulokozi alibainisha matatizo yatokanayo na kutotekelezwa kwa sheria hiyo, ikiwa ni pamoja na kwa waandishi, wasanii na wavumbuzi kutonufaika na kazi zao licha ya nguvu kubwa na ubunifu wanaotumia kwa miaka kadhaa mpaka kufanikisha upatikanaji kazi husika kitu kinachovunja moyo.

“Nina vitabu vyangu nimeandika vinatumika na silipwi chochote,” alisema. Alisema kutotekelezwa kwa sheria kunatokana na sababu nyingi ikiwemo uelewa mdogo miongoni mwa wasanii, wavumbuzi na waandishi, hivyo kupoteza haki zao kirahisi kwa kutofuatilia pale ambapo wanadhulumiwa.

Alisema tatizo ni kubwa nchini hususani kwenye taasisi za elimu ya juu na miongoni mwa wanataluma katika ngazi mbalimbali ambao hutumia kazi za waandishi wengine bila kuzingatia wanapata nini.

Alisema kampuni za uchapishaji mara nyingi zimekuwa zikiandika mikataba kwa lugha ya Kiingereza ambayo haieleweki na watanzania, hivyo kutumia udhaifu huo kuwadhulumu waandishi kirahisi ambao husaini hata bila kuelewa au kushirikisha wanasheria.

“Unaweza kukuta wanataaluma, wanafunzi na wachapishaji wanarudufu nakala za kazi za waandishi na kuziuza bila kuwa na makubalino ya mapato na mwandishi wa kazi husika,” alisema.

Alisema uwepo wa teknolojia unachangia katika wizi wa kazi za wasanii katika maandishi, video na sauti ambapo mtu anaweza kuchukua kazi hizo hata kwa simu janja.

Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Zamda Geuza alisema matatizo mengine ya kutotekelezeka kwa sheria hutokana na uelewa mdogo miongoni mwa waandishi, wavumbuzi na wasanii ambapo huingia mikataba wasiyo na uelewa nayo.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utafiti, Machapisho na Uvumbuzi ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Emmanuel Kigadye alisema malengo ya warsha hiyo ni kuhuisha utamaduni wa uandishi wa kitaaluma, wanataaluma na taasisi za elimu ya juu.

Chanzo: habarileo.co.tz