0

Ruby ‘amkuna’ Bella

Ruby ‘amkuna’ Bella

Mon, 9 Nov 2020 Source: HabariLeo

MSANII Christian Bella amemfagilia Hellen George ‘Ruby’ kwa kuendelea kufanya kazi ambazo zinaacha alama kwenye tasnia hiyo.

Bella amempongeza mwanadada Ruby siku chache baada ya kurudia kuimba wimbo wake wa ‘Yako wapi mapenzi’ kibao alichokiachia miaka 14 iliyopita na kupokelewa vizuri na mashabiki wake.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Bella alisema kitendo cha Ruby kurudia wimbo huo inaonesha bado anaheshimu kazi hiyo.

“Ruby ni msanii mzuri na amekuwa akifanya kazi ambazo zimekuwa zikiacha alama ya ujumbe mzuri na kitendo cha kurudia wimbo wangu wa yako mapenzi ni jambo jema ni kazi ambayo ilinipa heshima kubwa katika tasnia ya muziki Tanzania,” alisema Bella.

Bella alisema anashangaa kuona taarifa zikizagaa kwenye mitandao kutaka kuwagombanisha kwa sababu Ruby amerudia wimbo huo.

“Siwezi kugombana na Ruby tunaheshimiana toka muda mrefu na mara kadhaa nimekuwa nikimpatia ushauri namna ya kutengeneza kazi bora, naelewa kazi zake na yeye zangu anazikubali siwezi kugombana naye,” alisema.

Bella alisema wimbo huo ulikuwa wa taifa kwani watu wengi walimpongeza na walikuwa wanapenda kuusikiliza na kuuimba na kama msanii bado anajihisi furaha kuona jitihada zake zinatambulika.

Chanzo: HabariLeo