0

Rais Samia aikumbuka michezo, burudani

Rais Samia aikumbuka michezo, burudani

Tue, 6 Apr 2021 Source: Mwanaspoti

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameitazama Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na kuwaagiza wahusika kulitazama eneo hilo kwa mapana yake, ili kulipa nguvu, kutokana na vijana wengi wanapata ajira na kuipunguzia mzigo Serikali.

Katika hotuba yake ya leo Jumanne Ikulu ya Dar es s Salaam wakati akiwaapisha makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu wa wizara na wakuu wa taasisi mbalimbali aliowateua juzi Jumapili alizungumzia wizara hiyo kwamba liangaliwe kwa mapana yake kutokana na vijana wengi kupata ajira huko.

"Michezo na burudani kuna mambo mengi sana hapo, lakini niseme  jambo la msingi tuwape nguvu kwa mapana yake kwasababu vijana wengi wanajiajiri huku, hilo linaipunguzia  serikli mzigo mzito wa ajira kwa vijana, lakini pia tusisahau utamaduni wetu kwani tukienda nje, wanajua huyu ni Mtanzania," alisema .

Mbali na hilo alisisitiza kuhusiana na sheria za vyombo vya habari na kuwekwa wazi, kwamba inapotokea suala la kukifungia chombo cha habari kinachokiuka kanuni basi kinaelezwa kifungu cha sheria iliyotumika.

"Inapotokea chombo cha habari kinafungiwa basi inakuwa inaelezwa kimefungiwa kwa kosa hili, hilo linatakiwa kuwekwa sawa ili kuondoa maneno ya vyombo vya habari kukosa uhuru, tusivifungie kibabe hilo sio sawa," amesema.

Chanzo: Mwanaspoti