0

Mtoto wa Mengi kuendeleza utamaduni wa baba yake

Mtoto wa Mengi kuendeleza utamaduni wa baba yake

Mon, 2 Nov 2020 Source: HabariLeo

KAMPUNI ya IPP Ltd ya Dar es Salaam imesema, kuanzia mwakani itaendeleza utamaduni aliyouanzisha Mwenyekiti Mtendaji mwanzilishi wa kampuni hiyo Dk Reginald Mengi wa kula chakula na watu wenye ulemavu na utakuwa ya kudumu.

Mkurugenzi wa IPP, Abdiel Mengi alitoa ahadi hiyo katika hafla ya kupokea tuzo maalumu ya Dk Mengi kutambua mchango wake katika kusaidia jamii ya Watanzania.

Alikuwa akijibu hoja ya Elimringi Ngowi ambaye ni miongoni mwa watu walioathirika kwa polio na kunufaika bajaji aliyopewa na Dk Mengi.

Ngowi alisema utamaduni wa Dk Mengi uliwawezesha Watanzania kuwa karibu naye zaidi kwa kuzungumza naye na kucheza naye muziki.

Abdiel ni mtoto wa Dk Mengi. Mwaka 2011 Dk Mengi alitoa shilingi milioni 40 kusaidia kutokomeza ugonjwa wa polio.

Katika hafla hiyo mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa klabu ya Rotary ya Moshi, Arthur Kiwia alisema, Oktoba 24 2011 Dk Mengi alikuwa mgeni rasmi katika matembezi ya hisani ya kusaidia kupambana na ugonjwa wa polio na alitoa kiasi hicho cha fedha.

Alisema, fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti ya klabu ya kimataifa ya Rotary ili kusaidia kutokomeza ugonjwa huo.

Akikabidhi tuzo hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Nathanieli Mshana alimtaja Dk Mengi kuwa alikuwa mtu wa msaada katika jamii na kwamba kifo chake kiliacha pengo kubwa kwa jamii na taifa kwa jumla.

Baada ya hafla hiyo mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa klabu ya Rotary ya Moshi Dk Sadikiel Kimaro alikabidhi viti vinne vya magudumu manne kwa watoto wanne walioathirika na ugonjwa wa polio ili ziwasaidie.

Chanzo: HabariLeo