0

Mbinu 4 za kumfurahisha mwanaume

Mbinu 4 za kumfurahisha mwanaume

Mon, 5 Oct 2020 Source: HabariLeo

USHAURI wa aina nyingi umekuwa ukitolewa kuhusiana na jinsi ya kumfanya

mwanaume afurahie uwepo wake katika uhusiano.

Kubwa kati ya zinazotajwa ni pamoja na kumheshimu mume au 'boifrendi' wako na

kumfanyia matendo ambayo nawe ungelipenda kufanyiwa na kuachana na yale ambayo

hata wewe usingelipenda kufanyiwa.

Zifuatazo ni baadhi ya mbinu za ziada kuweza kumpatia mwanaume wako furaha

tarajiwa katika uhusiano.

1. MPE NAFASI YA UHURU AKIUHITAJI

Hata pale ambapo mwanaume wako amekuwa 'chizi' kabisa kimapenzi kwako,

anahitaji muda fulani kidogo wa kuwa peke yake kila wakati na hivyo hutakiwi kabisa

kulazimisha kuwa naye kwa saa 24!

Weka baadhi ya mipango pasipo yeye na mweleze ya kwamba yupo huru kutoka peke

yake, kunywa bia na rafiki zake au katika mazoezi ya jioni, vyovyote vile

anavyojisikia.

Hii pia hukupa nafasi ya kutimiza mambo yako binafsi na kuendeleza uhusiano

usiochosha.

Pindi unapokubali kwamba kila mmoja wenu anahitaji uhuru binafsi kila wakati,

utakuwa na furaha ya kuwa mapenzini na pia kuthaminisha ule muda wa kuwa pamoja

unapopatikana.

2. MZUNGUMZIE 'ISHU' ZOTE

Badala ya kusheheni majadiliano ya matukio ya ugomvi kila mara au matatizo ya

uhusiano wenu kila wakati, kaa chini na mwanaume wako kwa utulivu na unyenyekevu

mzungumzie mambo yenu yote kuanzia muhimu na yasiyo muhimu sana.

Ataheshimu hili na kuvutiwa kukusikiliza zaidi ikiwa ni pamoja na kutekeleza yale

unayomweleza na si kukupinga kila wakati.

Unatakiwa pia kuwa katika nafasi ya kutamka jambo lolote alilonalo au linalokusibu

wewe. Msikilize kwa dhati anachosema na usiingilie maongezi yake katikati na

kupinga au kubisha bila sababu za msingi.

Mwanaume wako atakuwa mwenye furaha kupitiliza katika uhusiano pale

atakapojihisi mawazo na hisia zake vina thamani kubwa kwako.

3. UPENDO KIDOGO, HESHIMA NYINGI

Wanaume wengi wa kisasa hujitahidi kutoa usawa kwa kuwafanyia wapenzi wao

majukumu saidizi katika kutambua umuhimu wa kusaidiana.

Wapo wanaowasaidia wenzi wako shughuli za jikoni, majumbani, ulezi wa watoto na

hata maandalizi ya watoto kwa maana ya safari za kliniki na kuwapeleka shuleni.

Heshimu hilo kwake na utambue thamani ya mchango wake huo na kukujali kwake

huko.

Usichukulie poa yale unachofanyiwa na mwanaume wako yawe makubwa au madogo

ukayaweka katika mzania kupima na kudhani ni stahili yako kufanyiwa hivyo.

Mjulishe thamani ya mapokeo ya wema anaokufanyia na jinsi anavyojaribu kufanya

kila awezalo kukusaidia na kukutimizia malengo.

Akikufanyia jambo fulani zuri, kuwa na shukrani stahiki. Mpe busu, mkumbatie

umweleze 'nakupenda'. Kujua kwake amekufurahisha kiasi gani, itamwongezea

furaha zaidi ya kuwepo katika uhusiano na wewe!

4. KUMBUKA: UHUSIANO NI MTAA WA NJIA MBILI

Uhusiano ni mtaa wenye njia mbili za kupishana. Hilo liko wazi kwamba kumfanya

mwanaume wako awe na furaha hakutakuwa na maana kama wewe binafsi hauna

furaha.

Uhusiano hufanya kazi kwa nafsi zote mbili kwahiyo kama utafanya jitihada zote

wewe mwenyewe pasipo majibu ya upande wa pili unatakiwa ufike pahala ujiulize

wewe mwenyewe kwamba "inalipa?"

Hata kama uhusiano wako unaendelea vizuri, kunaweza kuwa na mambo yanakwaza na

kukunyima furaha.

Inakubidi kutengeneza mapema ili usifike wakati wa mwenzi wako kubaini kwamba

huna furaha kwani na yeye ataanza kunyong'onyea na kukosa furaha hasa pale

atakapokosa kujua cha kufanya kutatua tatizo hilo.

Maoni 0713214724

Chanzo: HabariLeo