0

Maisha Magic Bongo yaadhimisha miaka 5 ya ‘Maajabu’

Maisha Magic Bongo yaadhimisha miaka 5 ya ‘Maajabu’

Tue, 6 Oct 2020 Source: HabariLeo

CHANELI maarufu ya Maisha Magic Bongo – DStv 160 ilizinduliwa rasmi Oktoba 2015 ikiwa na lengo kuu la kuyapa maudhui ya kitanzania jukwaa mahususi na kuwapa watazamaji burudani zenye ladha halisi ya Tanzania kuanzia lugha, Sanaa na utamaduni. Tangu wakati huo, chaneli hii imekuwa chaneli pendwa hapa Tanzania ikiwa na maelfu ya washabiki wanaoongezeka kila uchao.

Kumbukumbu ya mwanzo wa maajabu haya yametoka wapi?

“Chaneli hii mwanzoni ilikuwa mahsusi kwa ajili ya filamu pamoja na vionjo vya vipindi vya Maisha ya kila siku. Hata hivyo kadiri mahitaji ya watazamaji yalivyoongezeka chaneli hii iliongeza vipindi kama vile vya visa na mikasa, tamthilia, Telenovela bila kusahau tamthilia za kihindi zilizotafsiriwa kwa Kiswahili ambazo zinapendwa sana hapa Tanzania” amesema Barbara Kambogi, Mkuu wa Chaneli ya Maisha Magic Bongo.

Moja ya vipindi vilivyoipatia umaarufu mkubwa chaneli hii ni pamoja na Mzooka- kipindi cha muda was aa moja cha muziki kilichosheheni vigongo vipya vya wasanii nguli wa Tanzania, Talaaka- Tamthilia ya visa na mikasa iliyowagandisha watu mbele ya runinga zao, kipindi maalum cha mapishi - Jikoni na Marion kilichokuwa kikionyesha umahiri wa mapishi mbalimbali bila kusahau tamthilia pendwa za Kapuni na Sarafu!

Kwanini wamekuwa kinara wa Burudani za Kitanzania?

“Tunafanya kazi na wazalishaji maudhui mahiri kabisa ambao tumeshiriki katika kuwakuza na kuwawezesha kuzalisha maudhui yenye viwango vya kimataifa” alisema Barbara na kuongeza “Kwa miaka mitano iliyopita chaneli hii imefanyiwa maboresho makubwa huku ikijikita zaidi katika kuwapa watanzania mahitaji yao ya burudani wanayostahili huku ikiimarisha sekta ya burudani na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Huku ikisherehekea miaka mitano ya mafanikio makubwa, Maisha Magic Bongo imezindua filamu mbili mpya Nyavu na Slay Queen ambazo kwa sasa ni gumzo la jiji bila kusahau kipindi mahususi cha mahusiano cha Date My Family ambapo huwaonyesha mabachela jinsi wanavyochumbiana kupitia familia zao. “Kwa hakika chaneli hii imekuwa ni chimbuko la burudani za kitanzania na tunaendelea kuwahakikishia wateja wetu burudani isiyo na kikomo”

Tunaelekea wapi kutoka hapa tulipo?

“Chaneli hii imedumu kwa miaka mitano sasa. Hii si kwa kubahatisha bali tumepitia vipindi vigumu vya kiuchumi. Tunaendelea kutathmini matakwa na mahitaji ya wateja wet una kuhakikisha tunaendana na kile wanachotaka kwa kuwapatia maudhui wanayoyapenda huku tukihakikisha kuwa tunatoa kipaumbele kwa maudhui ya kitanzania”amesema Barbara. Chaneli hii pia ina timu ya manguli wa maudhui na masoko ambao muda wote hutathmini mahitaji ya soko na kuhakikisha kuwa watuwaangushi wateja wetu.

Mambo bado yanaendelea kuwa motomoto ndani ya Maisha Magic Bongo. Wateja wakae mkao wa kula kwani kuna vipindi vya kukata kwa shoka ikiwemo Jua Kali na Pazia ambavyo vyote vinatarajiwa kuanza mnamo Januari 2021. Huu si wakati wa kupepesa macho, tulia tuli ndani ya Maisha Magic Bongo kwa kwa vipindi maridhawa.

Chanzo: HabariLeo