0

Kikongwe wa miaka 97 aoa mzee wa miaka 73 

F911ec1505e426c27fe96068d68d859a.png Kikongwe wa miaka 97 aoa mzee wa miaka 73

Mon, 5 Oct 2020 Source: habarileo.co.tz

KIKONGWE James Tumbo (97), mkazi wa kijiji cha Usoke Mlimani Kata ya Uyumbu wilayani Urambo mkoa wa Tabora, amefunga ndoa na mwanamke aliyeishi nae kwa miaka mingi Sophia Jumali (73).

Wenza hao wameoana katika ibada ya ndoa, iliyofanyika nyumbani kwa Tumbo eneo la Ichencha.

Baada ya ibada, bwana harusi alisema ameamua kumuoa Sophia ili kumshukuru, kwa kuwa wameishi pamoja kwa muda mrefu, na pia kuifundisha jamii, kuwa umri si kigezo cha kuacha kufunga ndoa.

"Nimemuoa Sophia kwa kuwa tumeishi miaka mingi akiwa mlezi wa familia yangu yenye watoto sita kwa sasa, wa saba alifariki, hii iwe fundisho kwa jamii nzima kuwa na upendo kwa wenza wao na kuonesha ndoa hufungwa wakati wowote"alisema Tumbo.

Alisema jamii inapaswa kuzingatia miongozo ya dini, ili kuepuka migogoro ya familia inayosababisha ndoa.

Alisisitiza kuwa wanandoa, wana wajibu wa kuvumiliana kwenye shida na raha na uzima na ugonjwa.

Mtoto wa tano wa Tumbo, Yusto James (67) alisema vijana wanapaswa kuepukana tabia ya kuoa na kuacha, kwa kuwa hali hiyo kusababisha migogoro.

"Kumekuwa na kasumba ya vijana kuoa na kuacha, leo baba yangu ametufundisha kuwa kuna matunda ndani ya uvumilivu kwenye ndoa. Mama yetu mlezi ametulea katika shida na raha na leo amekamilisha kile kilichoagizwa na Mungu"alisema mtoto wa mzee huyo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ichecha, Omary Muhamed aliitaka jamii kujifunza kuwa ni vyema kuishi katika misingi ya imani ya dini, kwa kufunga ndoa na kufuata maagizo ya Mwenyezi Mungu.

Alisema kwene eneo hilo, kuna vijana wengi wenye tabia ya kuchukuana na kuishi kama mke na mume bila kufunga ndoa. Alisema hali hiyo inachangia kuporomoka maadili.

Chanzo: habarileo.co.tz