0

Jide One Time freshi!

Jide One Time freshi!

Fri, 23 Oct 2020 Source: Mwanaspoti

By KELVIN KAGAMBO HUKO mtandaoni kulichafuka, baada ya kuzuka kwa taarifa kwamba Comando, Lady Jaydee ukipenda muite Jide goma lake jipya la One Time limepigwa pini, lakini Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), limekata mzizi wa fitina na kuweka bayana kwamba hakuna kitu kama hicho.

Basata imezikanusha taarifa zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini kwamba limefungia wimbo wa Lady Jaydee wa One Time kupitia taarifa yao kwa umma waliyoitoa Oktoba 21 kwa kufafanua waliuzuia wimbo huo kuchezwa, lakini wakimtaka Jide aufanyie marekebisho na sio kuufungia.

“Baraza lilimuita msanii husika na kufanya naye kikao na kumpa maelekezo ya kufanya ikiwamo kufanya maboresho ya wimbo husika na kuuwasilisha Baraza kusikilizwa na kupewa daraja ili uweze kupelekwa kwa walaji,” inasomeka sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Ofisa Habari Mwandamizi wa baraza hilo Agnes Kimwaga.

Baadhi ya vyombo vilivyoripoti taarifa hiyo iliyokanushwa na Basata viliandika kwamba msanii huyo amepokea barua kutoka baraza ikimjulisha kuwa imefungia wimbo huo huku ikiwa haionyeshi kosa.

Oktoba 16 gazeti hili lilifanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza ambaye alithibitisha kwamba walimuita msanii huyo mwenye majina mengi ikiwamo Anaconda, Dada Mkuu na Binti Machozi kwa ajili ya mahojiano.

“Ni kweli tumemuita Jaydee kama wazazi na walezi wake katika sanaa kwa ajili ya mahojiano, kubwa likiwa ni wimbo wake wa One Time, kwenye video kuna kitu kama bangi anaonekana akivuta.” alisema Mngereza.

Chanzo: Mwanaspoti