0

Balaa MC aomba kukutanishwa na Polisi aliyeimba ‘Nakuja’

Thu, 5 Nov 2020 Source: mwanaspoti.co.tz

By NASRA ABDALLAHMsanii wa nyimbo za singeli, Balaa MC, ameomba yoyote atakayemuwezesha kumkutanisha na polisi aliyeimba wimbo wake wa ‘Nakuja’ kufanya hivyo, kwa kuwa anatamani kumuona ana kwa ana.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku mbili zimepita tangu kusambaa kwa video ikiwaonyesha baadhi ya polisi wakiwa wanaimba wimbo wake huo, wimbo ambao unafanya vizuri kwa sasa kwa upande wa muziki wa singeli.

Balaa MC alitoa ombi hilo leo Jumatano Novemba 4, 2020 alipotembelea ofisi za kampuni ya Mwananchi maeneo ya Tabata Relini, ambapo pamoja na mambo mengine aliyozungumza katika mahojiano, alichomekea na suala hilo.

Alisema sababu ya kumtafuta Polisi huyo ni kumpa shukurani namna alivyouthamini hadi kuuimba wimbo huo na kuongeza kwamba hii ni namna gani muziki huo sasa umekubalika vilivyo na watanzania.

“Kiukweli sijui nisemaje baada ya kuona clip ile ya Polisi tena wakiwa wameshika silaha zao na kuimba na wimbo wangu, imenifanya nami nijione shujaa kama wao, kwa yeyote anayemfahamu Polisi yule aliyekuwa akiwaimbisha wenzake naomba anikutanishe naye,”ameomba Balaa MC ambaye jina lake halisi ni Hussein Mashaka.

Wimbo wa Nakuja ulitoka miezi sita iliyopita lakini umezidi kujulikana zaidi ulipotolewa remix wiki mbili zilizopita ambapo Balaa MC alishirikiana kuimba na msanii wa Bongo Fleva, Marioo.

Chanzo: mwanaspoti.co.tz