0

Watendaji waagizwa wawe watiifu kwa Muungano

Watendaji waagizwa wawe watiifu kwa Muungano

Wed, 7 Apr 2021 Source: HabariLeo

RAIS Samia Suluhu Hassan ametaka mawaziri na makatibu wakuu kuwa watiifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushirikiana na wenzao wa Zanzibar katika sekta husika ili kujenga taifa.

Aliyasema hayo baada ya kuwaapisha makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na wakuu wa taasisi mbalimbali Ikulu, Dar es Salaam. Aliwateua kushika nyadhifa hizo mwishoni mwa wiki.

Alisema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa inafanya kazi kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwa jamhuri ni pande mbili za Muungano (Tanzania Bara na Zanzibar), hivyo lazima kufanya kazi kwa manufaa ya pande zote mbili.

Alisema katika viapo vyao amewasikia wakiapa kuwa watiifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ingawa katika muundo kuna serikali mbili inatakiwa kuwajibika kwa kuhakikisha pande zote mbili mambo yanaenda sawa.

“Naomba mind (akili) zenu zikae hivyo kuwa mnafanya kazi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hili ni kwa mawaziri na makatibu wakuu wote,” alisema Rais Samia.

Alisema katika kushirikiana ni suala jepesi kwa upande mmoja kushirikiana na mwenye sekta kama yake wa upande wa pili ili mambo yaende vizuri na hakuna sababu ya kuwekeana vigingi kwa “kuona hii ya nini…Zanzibar…Wazanzibar nao wamezidi weka hapa.”

Alisema Wizara ya Mambo ya Nje kwa sasa amempeleka mwanamke, Balozi Liberata Mulamula ambaye ni mwanadiplomasia na anajua masuala ya mambo ya nje huku Katibu Mkuu Balozi Kanali Wilbert Ibuge anayeijua vizuri wizara hiyo kutokana na kuwakilisha nchi katika masuala mbalimbali.

Lakini aliaidi kutafuta Mkuu wa Itifaki ili kumsaidia kazi katibu mkuu kufanya wajibu wake. Balozi Ibuge alikuwa pia Mkuu wa Itifaki katika wizara hiyo.

Rais alisema kazi kubwa iliyopo ni kukuza mahusiano na mataifa ya nje kutokana na waziri huyo kusikilizwa na mataifa ya nje na amefanya kazi nao na kuwataka kwenda kuweka mahusiano mazuri na mataifa ya nje

“Kuna msemo unasema ukitaka kufika haraka nenda peke yako lakini ukitaka kufika mbali nenda na wenzio…sasa unafika haraka kwa lengo ulilokusudia hatutaki kwenda peke yetu twende na wenzetu naomba mkarekebishe haya,” alisisitiza Rais Samia.

Chanzo: HabariLeo