0

Wezi wavunja kanisa, waiba kikombe cha ekaristi, divai

Wezi wavunja kanisa, waiba kikombe cha ekaristi, divai

Fri, 12 Mar 2021 Source: HabariLeo

WATU wasiojulikana wamevunja Kanisa Katoliki Parokia ya Wanging'ombe Jimbo la Njombe mkoani Njombe na kuiba vifaa vya ibada vinavyokadiriwa kuwa na thamani ya kati ya Sh milioni mbili hadi tatu.

Akizungumza na HabariLEO jana, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa jimbo hilo, Padri Innocent Chaula alivitaja vifaa hivyo kuwa ni vyombo viwili vya kuhifadhia ekaristi takatifu na kinachotumika kuhifadhia divai.

Vingine ni kikombe cha ekaristi, sahani ya kuwekea hostia (mkate) kubwa kwa ajili ya mapadri, shati inayovaliwa na padri na kifaa cha kuchomea ubani.

Padri Chaula alisema vyombo hivyo vina rangi ya dhahabu na huenda walioshiriki katika wizi huo walijua vimetengenezwa kwa madini hayo ya thamani kabla ya kuamua kuviiba na kutokomea navyo.

“Vyombo hivyo vimepakwa rangi ya dhahabu, ukiviangalia kwa haraka haraka unaweza kudhani vimetengenezwa kwa dhahabu halisi lakini sio,” alisema Padri Chaula.

Akizungumzia tukio hilo lilivyotokea, alisema lilitokea usiku wa kuamkia Machi 9, mwaka huu.

Alisema watu hao wasiojulikana waliingia kanisani baada ya kuvunja moja ya madirisha, wakaingia katika chumba cha maandalizi ya shughuli za ibada na kuiba vifaa hivyo.

Alisema kuibwa kwa vifaa hivyo kutaathiri kwa kiwango fulani shughuli za parokia hiyo zikiwemo ibada za vigangoni. Alisema parokia hiyo yenye waumini zaidi ya 3,500 inahudumia vijiji 16.

“Huduma zingine za kanisa zinaendelea kama kawaida wakati taratibu za kupata vifaa vingine na kuvitafuta vilivyoibiwa zikiendelea,” alisema Padri Chaula.

Alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuchukua hatua za haraka kushughulikia suala hilo ambalo uchunguzi unaendelea. Alisema wana imani Polisi itafanya kazi yao kwa weledi ili wahusika wapatikane na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Chanzo: HabariLeo