0

Takukuru yachunguza viongozi wakuu wa Kanisa EAGT

Takukuru yachunguza viongozi wakuu wa Kanisa EAGT

Wed, 17 Feb 2021 Source: HabariLeo

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inachunguza malalamiko ya vitendo vya rushwa, wizi na ufisadi, vinavyodaiwa kufanywa na viongozi wakuu wa Kanisa la Evangelical Assemblies of God of Tanzania (EAGT).

Taarifa ya Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani, ilieleza jana kuwa zaidi ya wachungaji 540, wanalalamikia vitendo hivyo ukiwemo uingizaji wa zaidi ya magari 50 na pikipiki kwa jina la kanisa na kusamehewa kodi, lakini kanisa halivitambui na halijawahi kuvipokea.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Takukuru imehoji baadhi ya walalamikaji, imekusanya vielelezo na inaendelea kuwaita walalamikiwa.

“Na leo hii Februari 16, 2021 tumemhoji Askofu Mkuu wa kanisa hilo Askofu Abel Mwakipesile”alieleza Kapwani na kubainisha lengo la uchunguzi huo ni kufahamu ukweli kuhusu malalamiko hayo ili hatua zichukuliwe.

Pia viongozi wakuu wa EAGT wanatuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha na mali ya kanisa katika mkataba kati ya kanisa hilo na wapangaji, duka la Imalaseko Supermarket Investment.

Inadaiwa kuwa mapato yanayotokana na majengo hayo, hayajawekwa wazi hivyo kuashiria kuwepo kwa ubadhirifu.

Tuhuma nyingine ni ubadhirifu wa fedha za kanisa kwenye ununuzi wa shule iitwayo Oasis Education and Community Development iliyopo Kahama.

Taarifa hiyo ya Kapwani ilieleza pia kuwa inadaiwa kuna Namba za Mlipa Kodi (TIN) zaidi ya tano zilizosajiliwa kwa jina la Kanisa la EAGT na zimetumika kuingiza magari kwa jina la kanisa na kusamehewa kulipa ushuru wa forodha wakati magari hayo hayajanunuliwa na kanisa.

Pia inadaiwa kwa mapato na matumizi ya kanisa, haviwekwi wazi na pia kanisa halina kitengo cha ukaguzi wa ndani.

Kwa mujibu wa Takukuru, baadhi ya tuhuma hizo zinaangukia chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Chanzo: HabariLeo