0

Serikali yataka kasi uchunguzi kesi za ubakaji

Serikali yataka kasi uchunguzi kesi za ubakaji

Wed, 3 Mar 2021 Source: HabariLeo

NAIBU Waziri, Ofi si ya Rais, Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuongeza kasi ya uchunguzi na ufuatiliaji kesi za ubakaji na mimba za utotoni ambazo zimekuwa zikiwanyima haki waathirika wa madhira hayo kutimiza ndoto zao za baadaye.

Naibu Waziri alitoa kauli hiyo jijini hapa jana wakati akizungumza na watumishi wa Takukuru wa nchi nzima waliokusanyika jijini hapa. Ndejembi alisema hivi karibuni serikali imegundua kuwa kumekuwa na mtindo ambao sio mzuri kesi nyingi zinazohusu rushwa ya ngono, ubakjaji, na mimba za utotoni zimekuwa zikiharibika na kupoteza ushahidi.

“Serikali imejipanga kuhakikisha kesi zote zinazohusu rushwa ya ngono aendelezwa na kama kuna mzazi atabainika na kosa la kumaliza kesi hizo atachukuliwa hatua kwa sababu sheria ipo inayomtaka kila mzazi kutimiza wajibu wake.

“Nasisitiza kama kuna mzazi anafanya hivyo atambue kuwa anafanya kosa kisheria na wanakuwa wanalea kosa la rushwa ya ngono na ubakaji kuendelea kushamiri katika jamii,”alisema.

Ndejembi aliwaagiza Takukuru katika mipango mikakati yao ya mapambano ya rushwa kuelekeza kwenye vyuo vyote nchini kuhakikisha wanamaliza suala la rushwa ya ngono ambako kwa kiasi kikubwa imeshamiri.

“Mmefanya vizuri kwenye utafiti mliofanya ndani ya vyuo vikuu viwili Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) huu ni wakati mwafaka wa nguvu zenu mkazielekeza kwenye vyuo vyote nchini kwani bado tatizo la rushwa ya ngono lipo,”alisema Ndejembi.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo alitaja mipango mikakati ya miaka mitano ijayo kuwa ni kuhakikisha wanatekeleza Ilani ya CCM ikiwamo kuboresha mfumo wa utendaji kazi katika maeneo mbalimbali.

Alisema katika awamu hii ya pili sasa ni wakati wa kutekeleza maagizo yanayotolewa na Rais John Magufuli na kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake bila kuonewa wala kudhurumiwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Bilinith Mahenge aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kusimamia na kuziba mianya ya rushwa kwenye sekta mbalimbali nchini.

Chanzo: HabariLeo