0

Polisi waua majambazi 5 Dar

Polisi waua majambazi 5 Dar

Tue, 2 Mar 2021 Source: HabariLeo

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeua majambazi watano, waliokuwa wanakwenda kufanya uhalifu maeneo mbalimbali.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema jana kuwa katika tukio hilo askari mmoja akijeruhiwa, na pia Polisi walikamata bastola aina ya Star iliyofutwa namba ikiwa na risasi tatu na maganda mawili ya risasi.

Kamanda Mambosasa aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Polisi waliua majambazi hao Februari 27 mwaka huu saa 12:00 asubuhi maeneo ya Kivule Kwa Iranga wilaya ya Ilala.

Alisema jeshi hilo kupitia kikosi cha kupambana na ujambazi, liliua majambazi waliokuwa kwenye gari lenye namba za usajili T 836 DHF aina ya Toyota Noah.

Kwa mujibu wa Mambosasa, majambazi sita walikuwa kwenye gari hilo, wakienda kufanya uhalifu maeneo mbalimbali mkoani humo.

"Kabla hawajatimiza lengo lao, kikosi kazi cha Jeshi la Polisi kiliweka mtego na kufanikiwa kuzuia ujambazi huo kwa kutaka kuwakamata wahalifu hao, lakini majambazi hao walitoka kwenye gari na kuanza kukimbia huku wakiwarushia askari risasi na hatimaye askari walijibu mapigo na kufanikiwa kuwapiga risasi majambazi watano ambao walifariki dunia papo hapo na jambazi mmoja alifanikiwa kukimbia huku akifyatua risasi hovyo na kumjeruhi askari mmoja," alisema.

Mambosasa alisema baada ya kuwapekua, walikuta bastola moja ikiwa na risasi tatu ndani ya kasha na maganda mawili ya bastola. Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali yaTaifa Muhimbili.

Katika tukio lingine, Kamanda Mambosasa alisema jeshi hilo lilikamata watuhumiwa 10 wakiwa na pikipiki 16 zinazodhaniwa ziliibwa.

Alisema kuanzia Februari Mosi hadi 28, mwaka huu jeshi hilo lilifanya operesheni, kuwasaka wezi wa pikipiki na lilikamata watuhumiwa hao.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Stephen Paul (38) mkazi wa Ulongoni A, Salum Mustafa (28 mkazi wa Kigogo, na Nsajigwa Kaisi (25) mkazi wa Mongo la Ndege A.

Kamanda Mambosasa alisema Polisi walifanya operesheni hiyo, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa waaathirika wa matukio hayo, yaliyodaiwa kukithiri katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Alisema watuhumiwa hao wamekuwa wakiiba pikipiki katika maeneo mbalimbali na kuzipeleka kwa madalali ili kuziuza.

"Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na pikipiki zifuatazo: MC 967 CRT, MC 922 CSL, MC 646 CMS, MC 900 CRC, MC 218 CSP, MC 339 CRQ, MC 677 CNQ, MC 804 CRU, MC 271 CPT, MC 618 CRC, MC 885 CKB, MC 543 AWN na MC 735 CMF, zote ni aina ya Boxer; na pikipiki zenye namba za usajili MC 832 CQF, MC 634 CKA na MC 412 CKP aina ya TVS," alisema Kamanda Mambosasa.

Chanzo: HabariLeo