0

Polisi wachunguza gharama za tiba hospitali ya Aga Khan

Polisi wachunguza gharama za tiba hospitali ya Aga Khan

Fri, 19 Feb 2021 Source: HabariLeo

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imeanza uchunguzi kuhusu malalamiko ya wananchi juu ya gharama kubwa za matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo ya kupumua (pneumonia) baada ya kupokea malalamiko mengi.

Kamanda wa Polisi kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema jana kuwa, jeshi hilo limepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi dhidi ya hospitali ya Aga Khan ya jijini Dar es Salaam kuwa inatoza gharama kubwa za matibabu kwa wagonjwa wa pneumonia unaosababisha matatizo ya upumuaji.

Alisema Polisi baada ya kupokea malalamiko hayo imefungua jalada la uchunguzi lenye kumbukumbu namba DSMZ/CID/PE/34/2021.

Alisema malalamiko mengine ni wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika hospitali hiyo wakifariki dunia kumekuwa na tabia ya kuzuia miili ya marehemu na kudai kiasi kikubwa cha fedha kinyume cha maelekezo ya serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Kamanda Mambosasa alisema uchunguzi huo utakapokamilika na kubaini ukweli wa tuhuma hizo, hatua za kisheria zitachukuliwa na jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na Wizara ya Afya dhidi ya hospitali hiyo.

Katika tukio jingine, Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam imeua majambazi wawili na kukamata silaha moja aina ya shortgun yenye namba MO1562004 ikiwa na risasi mbili ndani ya kasha.

Alisema, Februari 17 mwaka huu zilipokelewa taarifa za siri kuwa kuna majambazi wamepanga kuvamia duka la wakala wa benki na mitandao ya simu maeneo ya Kimara Stop-over kwa kutumia pikipiki mbili.

“Ndipo Polisi kupitia kikosi maalum cha kupambana na uhalifu waliwafuatilia majambazi hao wakiwa njiani ma walipogundua kuwa wanafuatiliwa na askari walianza kurusha risasi hovyo.

Alisma Polisi walijibu mashambulizi hayo na kufanikiwa kuwajeruhi majambazi wawili na wengine wawili kutokomea na pikipiki mbili kusikojulikana,” alisema. Kamanda Mambosasa alisema baada ya upekuzi katika eneo la tukio ilipatikana silaha hiyo na maganda matano ya risasi ya bastola waliyokuwa wakiitumia.

Alisema majambazi hao ambao umri wao unakadiriwa kuwa kati ya miaka 30-40 walipelekwa Hospitali ya Mlonganzila na daktari alibaini kuwa wamefariki baada ya kuvuja damu nyingi.

Katika tukio jingine, Kamanda Mambosasa alisema silaha aina ya bastola iliyokuwa inamilikiwa na Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM) iliyoibwa Februari 15, mwaka huu, majira ya saa 11:00 alfajiri nyumbani kwake maeneo ya Kawe Beach imepatikana.

Alisema bastola hiyo aina ya Glock 17 yenye namba YX647 ikiwa na risasi 14 ndani ya kasha lake ilikamatwa juzi Februari 17 mkoani Mbeya baada ya ushirikiano wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na Polisi Mkoa wa Mbeya.

Alisema mtuhumiwa mmoja anashikiliwa kwa tuhuma za wizi wa silaha hiyo.

Chanzo: HabariLeo