0

Mtuhumiwa mauaji ya wanawake anaswa

Mtuhumiwa mauaji ya wanawake anaswa

Thu, 18 Feb 2021 Source: HabariLeo

JESHI la Polisi mkoani Arusha limemkamata anayedaiwa kuwa kiongozi wa mtandao wa mauaji ya wanawake mkoani humo, hasa kwenye Kata ya Mateves wilayani Arumeru.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Salumu Hamduni alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Mbise Sanare Lukumo (30).

Kwa muda mrefu Polisi walikuwa wakimtafuta kijana huyo mkazi wa Olasiti jijini humo.

Kamanda Hamduni alisema Lukumo alikamatwa Januari 27 mwaka huu na baada ya kuhojiwa, alikiri kuhusika na matukio ya mauaji ya wanawake kutokana na imani za kushirikiana.

Kamanda alisema miongoni mwa matukio ya mauaji yaliyofanywa na mtuhumiwa huyo ni kuuawa kwa mwanamke, Anna Edward (44) mkazi wa Kona ya Kiwanda Cha A to Z.

Januari 30 mwaka huu mwili wa mtu huyo ulikutwa kando ya nyumba yake ukiwa uchi wa mnyama.

Kamanda Hamduni alitaja matukio mengine ni la Mei 21 mwaka 2019 katika eneo la Lolovono, Arusha ambako mtuhumiwa huyo akiwa na wenzake wanatuhumiwa kumuua Stella Daniel (22) mkazi wa jijini humo.

Alisema, Januari 16 mwaka jana aliuawa Bahati Prosper (35), mkazi wa Ngaramtoni.

Kwa mujibu wa Kamanda Hamduni, mtuhumiwa huyo na wenzake walikiri kuhusika kumuua mwananchi huyo.

Alisema, baada ya kuhojiwa mtuhumiwa aliwataja washitakiwa wenzake akiwemo mganga wa kienyeji, Bashiri Msuya mkazi wa Kirika B, na Lembeka Olomorojo (65), wote wakazi wa Kata ya Osunyai jijini Arusha.

Kamanda Hamduni alisema watuhumiwa walidai kuwa wamekuwa wakihusika na mauaji hayo kutokana na imani za kishirikina, baada ya kushawishiwa na waganga wa kienyeji ili wapate utajiri.

Wakati huo huo Jeshi hilo kwa kushirikiana na Kikosi Cha kudhibiti Ujangili (KDU) Kanda ya Kaskazini kilicho chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA), katika kipindi Cha mwaka 2010 hadi 2020 walikamata silaha haramu zapatazo 125.

Kamanda Hamduni alisema, kati ya silaha hizo, za kutengeneza kienyeji ni magobore 125 na silaha moja aina ya semi Automatic Rifle, zote zinadaiwa kuhusika kwenye uwindaji haramu.

Kamanda wa KDU Kanda ya Kaskazini, Panjoko Peter, alisema kukamatwa kwa silaha hizo ni mkakati wa kutokomeza vitendo vya ujangili katika Kanda ya Kaskazini.

"Iwapo silaha hizo zote 126 zingeachwa ziendelee kutumika kwenye ujangili ni wazi kwamba matukio ya ujangili yangekuwa mengi na wanyamapori wangeuawa sana, jambo ambalo lingeathiri uchumi wa nchi"alisema

Chanzo: HabariLeo