0

Mmoja adakwa, wengine wasakwa uzushi afya ya JPM

Mon, 15 Mar 2021 Source: www.habarileo.co.tz

POLISI Mkoa wa Kipolisi Kinondoni imesema inawasaka watu wanaosambaza uvumi mitandaoni kuwa Rais John Magufuli ni mgonjwa na kwamba mtu mmoja, fundi simu aitwaye Charles Majura (35) anashikiliwa.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Ramadhani Kingai, alithibitisha kushikiliwa kwa Majura kwa kosa hilo na kwamba wanaendelea kuwasaka wote wenye tabia ya kusambaza taarifa za uzushi wakati kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa mkoani Pwani baada ya kikao cha makamanda wa Polisi wa mikoa minne ya Pwani, Morogoro, Tanga na Kinondoni.

“Watu wanaosambaza taarifa za uongo na za uzushi katika mitandaoni ya kijamii kuwa rais ni mgonjwa, taarifa zinazoleta hofu kwa wananchi. Taarifa hizi tumeanza kuzifuatilia na tarehe 11.3.2021 tulifanikiwa kumkamata mtu mmoja anayeitwa Charles Deus Majura ambaye alikuwa kinara wa kusambaza taarifa hizi.

“Tulimkamata ili aweze kushughulishwa kisheria, tunae, tunaendelea na mahojiano naye lakini pia kuendelea kukusanya ushahidi kuhakikisha kwamba anapelekwa mahakamani kujibu kosa hilo,” alisema Kamanda Kingai.

Alisema bado wanawasaka watu wengine wanaosambaza taarifa hizo za uzushi na yeyote anayefanya hivyo kueneza taarifa za hofu, watamsaka kokote na kumtia nguvuni.

“Niwoambe Watanzania wengine ambao hawajui sababu kutofahamu sheria si kinga ya kushitakiwa, ukikutana na taaifa ya uzushi kwenye mtandao usisambaze ni kosa. Taarifa hizo za kizushi tutazifanyia kazi na wahusika watakamatwa kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz