0

Mfanyabiashara, wasichana kortini kwa kilogramu 30 za heroin

Mfanyabiashara, wasichana kortini kwa kilogramu 30 za heroin

Fri, 12 Mar 2021 Source: HabariLeo

MFANYABIASHARA Said Mbasha (24) na wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kujihusisha na kilogramu 30.6 za dawa za kulevya aina ya heroin.

Mbali na Mbasha, washitakiwa wengine waliopandishwa kizimbani jana ni Joseph Dalidali (27), Allu Murungwa (24) na Fatuma Shomari (24) wote wakazi wa Kinondoni, Dar es Salaam.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya, kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka mawili ya kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Wakili Simon alidai kuwa Machi 3 mwaka huu katika eneo la Kijitonyama, Mkoa wa Dar es Salaam washitakiwa wote walijihusisha na kilogramu 30.6 za dawa za kulevya aina ya heroin.

Katika mashitaka ya pili, ilidaiwa kuwa Machi 3 mwaka huu, katika mtaa wa Kasaba, Kinondoni Dar es Salaam, Mbasha na Fatuma walikutwa na dawa za kulevya aina ya bangi gramu 2.63.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamlika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ambapo ilipangwa Machi 24 mwaka huu.

Washitakiwa wote walirudishwa rumande kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayana dhamana na hasa kiwango cha madawa walichokamatwa nacho.

Wakati huohuo mfanyabiashara, Riddeny Nkomo jana alifikishwa katika Mahakama hiyo akikabiliwa na mashitaka mawili likiwemo la utakatishaji Dola 11, 550 za Marekani.

Nkomo alifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 20/2021 na Wakili wa Serikali, Neema Mushi.

Mushi alidai katika tarehe tofauti kati ya Juni 25 na Julai 8,2020 nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa na lengo la kudanganya alijipatia Dola za Marekani 11,550 kutoka kwa Cosmas Sabao kwa kumdanganya kwamba fedha hizo ni kwa ajili ya kununulia gari aina ya Mercedez Benz E.320 kitu ambacho alijua si kweli.

Katika shitaka la pili ilidaiwa, katika tarehe tofauti kati ya Juni 25 na Julai 8, 2020, ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Nkomo alijipatia Dola za Marekani 11,550 wakati akijua wakati akijipatia fedha hizo ni zao la kosa la udanganyifu.

Mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa. Hakimu Ruboroga aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 25, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Mshitakiwa alirudishwa rumande kwa kuwa mashitaka hayo hayana dhamana kisheria.

Chanzo: HabariLeo