0

Mashine 40 za kubeti zateketezwa Morogoro

Mashine 40 za kubeti zateketezwa Morogoro

Mon, 22 Feb 2021 Source: HabariLeo

BODI ya Michezo ya Kubahatisha (GBT) imeteketeza mashine 40 za kampuni ya Bonanza Trading iliyokuwa inamilikiwa na raia wanne China.

Mashine hizo ziliteketezwa kutekeleza hukumu ya Mahakama ya kesi ya uhujumu uchumi Namba 38 ya mwaka jana.

Wachina hao walitambuliwa kwa majina ya Bangshun Zheng ambaye ni fundi wa mashine za bahati nasibu za kampuni ya Bonanza Trading, Chen Maoan, Li Yu na Wang Zhen.

Walikuwa ni wafanyakazi wa kampuni hiyo iliyokuwa inajuhusisha na michezo ya kubahatisha kwenye manispaa ya Morogoro, Halmahauri ya Wilaya ya Morogoro, na wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani humo.

Raia hao wa China walitiwa hatiani baada ya kukutwa na fedha za sarafu za Tanzania zenye thamani ya Sh 97,841,460.

Katika hukumu Mahakama iliamuru fedha hizo zitaifishwe na pia mashine 40 zilizokuwa zikitumika kwenye michezo ya kubahatisha ziharibiwe.

Kazi ya kuziharibu mashine hizo ilifanyika hivi karibuni katika eneo la kuunguza taka Kihonda viwandani kwenye manispaa ya Morogoro na kushuhudiwa na maofisa wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka na Mahakama ya Mkoa wa Morogoro.

Mkuu wa Mashitaka Mkoa wa Morogoro, Neema Haule, alisema mashine hizo zilikamatwa Mei 9 mwaka jana katika nyumba waliyokuwa wakiishi raia hao wa China.

Alisema, Wachina hao pia walikutwa wamehifadhi sarafu kinyume cha sheria na walifunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.

Haule, alisema mashine hizo zilionekana hazikuwa na viwango kwa vile ziliendelea kutumia sarafu za Tanzania katika mashine hizo zikiwa zimetobolewa kama spea.

Alisema, Mahakama ilitoa amri pia baada ya upande wa mashitaka kuomba mashine hizo ziharibiwe chini ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania na pia Mahakama itasimamia zoezi hilo.

"Sarafu za Sh 200 ambazo ndizo zilikuwa nyingi, Sh 500 , Sh 50 na nyingine Sh 10 na kiwango cha uhifadhi wa sarafu hizo zilikuwa ni kubwa sana na walikuwa wamehifadhi kwenye makopo, vyombo vya plastiki na mifuko ya salfeti kitu ambacho kilikuwa ni kinyume cha utunzaji wa fedha "alisema Haule wakati wa zoezi la uteketezaji wa mashine hizo.

Mkurugenzi wa urejeshaji mali zinazohusiana na uhalifu kutoka ofisi ya taifa ya mashitaka, Poul Kadushi, alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa sheria mpya inayoelekeza kutaifisha mali zinazopatikana kwa njia ya uhalifu.

Alisema awali mshitakiwa alikuwa akimaliza kutumikia adhabu yake anarudi kutumia mali ambazo alizozipata kinyume na sheria.

Mei 9 mwaka jana aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo, aliamuru kukamatwa wa raia wanne wa baada ya kukutwa wakiwa wamehodhi mamilioni ya sarafu fedha ya Kitanzania ndani ya nyumba kinyume cha sheria.

Chanzo: HabariLeo