0

Madereva wa mabasi 10 wafungiwa leseni, kushitakiwa

Madereva wa mabasi 10 wafungiwa leseni, kushitakiwa

Fri, 2 Apr 2021 Source: HabariLeo

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amefunga leseni za madereva 10 wa mabasi yanayokwenda mikoani wakidaiwa kuvunja sheria za usalama barabarani.

Simbachawene alifunga leseni hizo kwa miezi mitatu kwa kuwa madareva hao walidaiwa kuendesha mabasi kwa mwendokasi wa kilometa 125 kwa saa.

Aliwaeleza waandishi wa habari jana jijini Dodoma kuwa hivi karibuni baadhi ya madereva walianzisha tabia ya kukiuka sheria za barabarani na hivyo kuhatarisha maisha ya abiria wanaotumia vyombo hivyo.

Simbachawene alisema ameliagiza Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, liwashitaki mahakamani madereva hao 10 na agizo hilo litekelezwe ndani ya siku 14 tangu.

Aliwataja madereva hao kuwa ni Allan Msangi wa Kampuni ya Kapricon wa basi lenye namba T 605 DJR linalofanya safari za Dar –Moshi anayedaiwa kuendelesha mwendo wa kilometa 125 kwa saa, Hussein Dudu wa Kimotco Intertrade inayofanya safari Arusha kwenda Musoma (T 520 CXE) kwa mwendokasi wa kilometa 125 kwa saa.

Wengine ni Seleman Seleman wa Al-Saed (T 313 DSO) linalofanya safari za DarKilombero kwa mwendo wa kilometa 103 kwa saa, Athuman Mnzava wa MB Coach safari za Dar-Arusha likiwa na mwendokasi wa kilometa 107 kwa saa, na Juma Simba wa Baraka Classic (T 340 DPW) ya Dar-Masasi kwa mwendo wa kilometa 107 kwa saa. Pia wamo Salum Salum wa Nice (T 121 DEA) safari za Dar-Tunduru mwendo wa kilometa 110 kwa saa, na Frank Massawe wa Machinga safari za Dar-Mtwara (T 694 DRB) kwa kilometa 95 kwa saa.

Wengine ni Innocent Thompson wa Ester Luxury linalofanya safari za Moshi-Dar kilometa 107 kwa saa lenye namba za usajili T 225 DTB, Naseeb Nassoro wa NBC Classic la Tabora –Kigoma (T 565 BED) na Maiko Mkindi wa Kilimanjaro Express linalofanya safari za Dar-Arusha (T 675 DHY) kwa mwendo wa kilometa 100 kwa saa.

Simbachawene amewaagiza wamiliki wa mabasi hayo wachukue hatua stahiki kwa madereva wao ikiwamo kuwakumbusha mara kwa mara umuhimu wa kufuata sheria barabarani.

Alisema kuanzia sasa kila mwezi atakuwa na utaratibu wa kutoa ripoti ya madereva wanaofanya vibaya na kuwapongeza wanaofanya vizuri.

Chanzo: HabariLeo