0

DPP aonya wanaocheza upatu

Tue, 16 Mar 2021 Source: www.habarileo.co.tz

MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga amewaonya wanaoshiriki katika biashara haramu ya upatu wajue wapo katika hatari ya kupoteza fedha zao na kushtakiwa mahakamani kwa kosa la kushiriki katika biashara hiyo.

Akizungumza jijini Dodoma jana, Mganga alisema washiriki katika biashara hiyo wajue watapoteza fedha zao kama wengine walivyopoteza zaidi ya Sh bilioni 42.5 baada ya serikali kutaifisha fedha hizo kutokana na kucheza upatu huo.

Kutokana na kucheza upatu, Deci ilitaifishwa Sh bilioni 16 pamoja na magari, nyumba, viwanja vilivyoenea nchi nzima kwa mwavuli wa dini wakisingizia kupanda mbegu, D9 Sh milioni 500, Refaro Africa takribani Sh bilioni nne, Mr Kuku Sh bilioni takribani sita, na International Marketingi System (IMS) Sh bilioni 16.

Mganga aliukumbusha umma kujihadhari na mipango hiyo ambayo imewahi kujitokeza siku za nyuma na kusabababisha wananchi wengi kupoteza fedha zao.

Mipango hiyo danganyifu iliyosababisha wananchi wengi kupoteza fedha zao kiwango kikubwa katika taasisi zikiwemo Rifaro Africa, IMS, D9, miradi ya Kuku kupitia Kampuni ya Mr Kuku na Development Entrepreneurship Initiative (DECI).

Mganga alisema kwa sasa mipango hiyo ya kidanganyifu inayotangazwa kupitia mikutano ya uhamasishaji pamoja na mitandao ya kijamii, inayosisha viongozi wa siasa, viongozi wa dini na hata waandishi, imeubuka kwa sura mpya kama biashara ya kimtandao na wananchi wanaalikwa kushiriki na kushawishi wengine kujiunga.

“Kampuni ya QNET Limited ni moja ya mfano hao,imefunguliwa nchini Hong Kong na inajihusisha na biashara ya kuuza bidhaa kwa njia ya mtandao kupitia anuani yao ya www.qnet.net,” alisema DPP Mganga.

Alisema kampuni hiyo, iliweka masharti mawili ya atakayejiunga na biashara yao, kwa kutakiwa kupata mafunzo ya kuwa mwanachama na mwanachama huyo analazimika kuwashawi watu wengine kujiunga na kununua bidhaa za kampeni hiyo na anayefanikiwa kushawishi wengine kujiunga anapewa ahadi ya kupata kamisheni.

QNET katika kulinda shughuli zake, Februari Mosi mwaka huu, ilimwandikia barua Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara na kumpa nakala DPP ikimtaka kutoa ulinzi kwa kampuni hiyo pamoja na kuhakikisha haibughudhiwi na vyombo vya mamlaka za serikali, jambo ambalo si kazi ya mkurugenzi wa mashtaka.

Mganga alisema DPP hawezi kulinda biashara inayofanywa na kampuni hiyo ambayo ni biashara haramu ambayo ni kosa la jinai. “Siwezi kulinda wahalifu ama kuweka mazingira mazuri ya wahalifu kuendelea kutenda vitendo vya kihalifu,” alisema.

Aliagiza vyombo vya upelelezi kufanya upelelezi wa kina pamoja kuwakamata na kuwahoji wahusika wa kampuni hiyo ambayo walitaka kutumia nafasi ya uongozi kulinda biashara haramu ya upatu.

Katika uchunguzi wake, pia amebaini kwamba kuna baadhi ya taasisi za serikali zimekuwa zikirejesha fedha kwa baadhi ya wanaodaiwa kuwa ni waathirika wa uhalifu huo wa upatu, hivyo akatoa maelekezo kwa vyombo vyote vya upelelezi kutorejesha fedha kwa watu wanaoshiriki katika makosa ya upatu.

“Utaratibu wa kurejesha mali kwa waathirika au kutaifisha mali zinazohusiana na uhalifu umeanishwa katika sheria mbalimbali. Kwa msingi huo, wale wote wanaotaka kurejesha fedha au mali kwa waathirika zinazohisiana na uhalifu lazima wafuate taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria,” alisema.

“Mipango hiyo inafanyika pasipo kupata idhini ama kibali kutoka kwa mamlaka za serikali au hawana ofisi rasmi zinazotambulika katika uendeshaji wa shughulizao,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz