0

Wawekezaji wa mashine za mkonge watakiwa haraka   

Wawekezaji wa mashine za mkonge watakiwa haraka

Sun, 15 Nov 2020 Source: HabariLeo

BODI ya Mkonge imesema ipo haja ya kutafuta wawekezaji kutoka nje ya nchi na ndani, ambao watawekeza katika ununuzi wa mashine za kisasa za kusindika zao hilo ili wakulima waweze kupata faida .

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Marium Nkumbi alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza ziara ya siku mbili ya mashamba matano ya mkonge yaliyopo mkoani Tanga.

Alisema licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kufufua zao hilo kwa kuongeza uzalishaji wa miche bora, ipo haja ya kuanza kutafuta wawekezaji wa mashine ili kukabilina na changamoto ya uchakavu wa mashine uliopo.

"Kuna uhitaji mkubwa wa kutafuta wawekezaji ambao wataweza kuweka mashine za usindikaji kwenye mashamba yetu, kwani majani mengi yamevunwa lakini kasi ya kuyachakata ni ndogo kutokana na uchakavu wa mitambo"alisema Mwenyekiti huyo.

Kaimu Mkurugenzi wa bodi hiyo, Saad Kambona alisema kuwa hali ya masoko imezidi kuimarika, tofauti na hapo awali, kwani0 wamekuwa wakipokea oda nyingi za zao hilo.

"Tumekuwa tukipokea oda nyingi kutoka mataifa ya nje, lakini changamoto kubwa ni uwezo mdogo wa uchakataji wa zao hili unaotokana na uduni wa mashine "alisema Kambona.

Hata Hivyo, alisema kuwa kutokana na kuimarika kwa masoko, bei ya mkonge kutoka Tanzania katika masoko ya nje, nayo imekuwa ikipanda tofauti na awali.

Chanzo: HabariLeo