0

Wauza mafuta Mwanza wataka uhusiano mwema na TRA

Wauza mafuta Mwanza wataka uhusiano mwema na TRA

Tue, 6 Apr 2021 Source: HabariLeo

WAFANYABIASHARA wa mafuta mkoani Mwanza wameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuimarisha uhusiano na wafanyabiashara ili kuongeza wigo wa walipa kodi na kuongeza pato la taifa.

Katibu Mkuu wa Wauza Mafuta Kanda ya Ziwa (TAPSOA), Ahmed Bisanga, alisema wana imani kubwa kwamba TRA ikitekeleza haraka agizo la Rais Samia, itaharakisha matumaini kwa wafanyabiashara wote wakiwamo wa mafuta na kuongeza matumaini katika sekta ya biashara.

“Tuna imani sana na Rais Samia; ninachoomba ni kwamba, kuwe na ukusanyaji wa kodi katika njia nzuri bila ubambikizaji wa kodi,” alisema Bisanga.

Katibu mkuu huyo alisema wauzaji mafuta ni walipa kodi wazuri kwa kuwa wengi na karibu wote, wanatumia mfumo wa kisasa wa ukusanyaji kodi kupitia mfumo wa mashine za kieletroniki (EFD).

“Katika sekta yetu ya mafuta, tunaona bado kodi zipo nyingi sana kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha) na halmashauri, unakuta Osha wanataka kodi ya afya na halmashauri nao wanakuja kudai kodi hiyo hiyo sasa mzigo unakuwa mkubwa…” alisema Bisanga.

Mfanyabiashara kutoka kituo cha Sasa Kazi Fuel Limited, Charles Mtatula, alisema bado zipo kodi nyingi kutoka halmashauri ukilinganisha na faida wanayoipata kutokana na kazi yao.

Alisema wana imani na utendaji wa Rais Samia kwa kuwa ni mchapakazi, msikivu na mwenye msimamo wa haki na kwamba mambo hayo, yakiongezwa na agizo lake, wanaamini TRA itatoa unafuu kwa wafanyabiashara wa mafuta.

Naye Yakoub Macgeorges alisema: “Suala la ulipaji kodi lilikuwa ni utata sana; Rais kasema TRA wanatakiwa kuwa karibu na wafanyabiashara pamoja na kuwa marafiki wa wafanyabiashara ili kutanua wigo wa ulipaji kodi.”

Akaongeza: “Kama alivyosema Rais Samia, TRA wajenge urafiki, badala ya kuweka uadui na wafanyabiashara kwa kuwa uhasama badala ya kuvutia walipa kodi, unawafukuza na kusababisha serikali kukosa mapato yake kupitia ukusanyaji kodi.”

Chanzo: HabariLeo