0

Watumishi waliopunguzwa kazi Swissports waanza kurejeshwa

Watumishi waliopunguzwa kazi Swissports waanza kurejeshwa

Fri, 2 Oct 2020 Source: HabariLeo

KAMPUNI ya kuhudumia ndege ya Swissport Tanzania imesema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita imerejesha shughuli zake mara mbili zaidi ya ilivyokuwa wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa covid-19.

Hata hivyo, imesema ingawa haijafikia shughuli za kabla ya mlipuko wa ugonjwa huo, imeanza kurejesha kazini wafanyakazi waliokuwa wamepunguzwa katika kipindi hicho.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni inayojihusisha na utoaji wa huduma katika Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro (KIA) na Dar es Salaam (JNIA) ya Swissport, Mrisho Yassin alibainisha hayo wakati akielezea safari ya miaka 35 ya kampuni hiyo nchini Tanzania tangu kuanza kwake rasmi Oktoba mosi Mwaka 1985.

“Covid-19 iliathiri, naweza kusema kampuni zote na katika sekta ya usafiri wa anga tuliathirika zaidi, shughuli zetu za kuhudumia ndege zilipungua hadi asilimia 20 na kuhudumia mizigo kulipungua hadi asilimia 40, lakini sasa shughuli za kuhudumia ndege zimerudi hadi asilimia 60 na mizigo zimefikia asilimia 80 ikilinganishwa na ilivyokuwa kabla ya Covid-19,” alisema.

Alisema wakati wa mlipuko wa ugonjwa huo, kampuni hiyo iliyokuwa na wafanyakazi zaidi 1,000 na baadaye ilipunguza wafanyakazi 250 ambao tayari kwa sasa imeanza kuwarejesha taratibu baada ya hali ya ugonjwa huo kutengamaa.

“Miongoni mwao leo (jana) tumerejesha wafanyakazi 86 na kadri siku zinavyokwenda tutaendelea kuwarejesha wengine, imani yetu hadi mwishoni mwa mwaka huu watakuwa wamerejea wote kwani hata shughuli zao huenda zikawa zimerejea kwa asilimia 100,” aliongeza.

Kuhusu biashara, alisema kwa jumla inarejea ambapo tayari wateja wao 2,218 wamerejesha safari zao na wawili, zikiwemo kampuni za Oman Air na Uganda Airlines ingawa miruko yao kwa wiki imepungua tofauti na awali huku ufanisi ukiongezeka siku hadi siku.

Yassin alisema Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) ndiyo mteja wake mkubwa kwani kabla ya covid-19 ilikuwa ikiruka zaidi ya mara 36 na wakati wa ugonjwa huo, miruko ilipungua na sasa hali imeanza kurejea kama zamani.

Aidha, alisema kampuni hiyo ambayo hivi karibuni ilitangaza kupata hasara ya Sh bilioni 1.23 kwa kipindi cha miezi sita, inamiliki Chuo cha Mafunzo ya Huduma za Ndege kinachochangia mapato.

Chanzo: HabariLeo