0

Wasichana 3000 kunufaika na mafunzo ya ujasiriamali

Wasichana 3000 kunufaika na mafunzo ya ujasiriamali

Tue, 13 Oct 2020 Source: HabariLeo

WASICHANA zaidi ya elfu 3000 wanatarajia kufaidika na mafunzo ya ujasiriamali,Afya ya uzazi,utunzaji wa fedha na stadi za maisha. Akizungumza katika warsha ya siku moja,mkurugenzi wa asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Sauti ya Wanawake Ukerewe,Sophia Donald alisema taasisi yao inatarajia kutoa mafunzo hayo kupitia mradi wa Imarisha wasichana.

Alisema mradi huo utawanufaisha wasichana kutoka mkoani Mwanza katika wilaya ya Ilemela kata za Nyakato,Nyasaka,Ibungilo,Kahama,Buswelu na Kiseke. Donald alisema mradi wao ulianza Januari mwaka jana na utadumu kwa miaka miwili na mpaka sasa ni wasichana 200 wamenufaika na mafunzo hayo.

Alisema kupitia mradi huo pia umekuwa ukipinga vikali unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto wa kike na unyanyasaji wa kingono. Mmoja ya wanufaika wa mradi huo,Sarah Frank kutoka kata ya Nyakato alisema kupitia mradi wa Imarisha wasichana ameweza kupata mkopo na umemsaidia kujiajiri katika kazi yake ya ufundi chereani. Aliwaomba wasichana wenzake wahakikishe wanaepuka vishawishi na kufanya kazi kwa bidii.

Ofisa vijana wa Halmashauri ya Manispaa ya wilaya ya Ilemela,Lucy Matenga aliwataka wasichana kuhakikisha wanajiamini na kuepuka mimba za utotoni kwani zimekuwa zikikwamisha ndoto zao. Alisema serikali imeendelea kutoa fursa nyingi kwa watoto wa kike.

Chanzo: HabariLeo