0

Wakulima wataka mikopo nafuu

Wakulima wataka mikopo nafuu

Fri, 13 Nov 2020 Source: HabariLeo

WAKULIMA wa zao la korosho katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, wameziomba taasisi za kifedha kuweka masharti rahisi ya upatikanaji mikopo kwa wakulima.

Wamesema kuondolewa kwa masharti magumu ya mikopo na usumbufu usio wa lazima, kutaimarisha kilimo na kuhudumia mashamba yao kwa wakati.

Walisema hayo hivi karibuni katika mafunzo ya siku mbili kuhusu kilimo bora cha zao la korosho, yaliyofanyika wilayani Korogwe. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Naliendele.

Mafunzo hayo yalilenga kuwapa washiriki teknolojia mpya za kilimo bora cha korosho kwa kupanda mbegu bora na kudhibiti wadudu waharibifu na magonjwa katika korosho. Lengo ni kuwa ifikapo mwaka 2025 Tanzania iwe na uwezo wa kuzalisha korosho tani milioni moja kwa mwaka kutoka tani 313,000 zinazozalishwa sasa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mashewa katika halmashauri hiyo, Abdallah Shemzungu, alisema serikali inatangaza kuwa kuna mikopo ya kilimo, lakini mikopo hiyo ina urasimu kwa sababu kilimo hufanyika katika mashamba na siyo mijini. Alisema wakopeshaji wanapodai hatimiliki za ardhi au mashamba huwa kikwazo kwao kupata mikopo.

Alisema hali hiyo imekuwa ikiwaumiza wakulima hao kutokana taasisi hizo kushindwa kulitendea haki kundi hilo.

"Sisi tulienda kama mtu mmoja mmoja na tukaandika mchanganuo wetu kumbe benki zinataka tuwe na hatimiliki…naishauri sana serikali itazame hii mikopo ya wakulima sababu mashambani ndio kuna wakulima, mijini hakuna wakulima kuna wafanyabiashara," alisema.

Aliongeza "Wenzetu wa mjini wanazo hati za nyumba, lakini sisi vijijini nyumba zetu hazina hati na tunahitaji tukope, nashauri serikali za vijiji ziwe na mamlaka ya kumthibitisha huyo mkopaji na aaminiwe kwa vigezo hivyo au masharti yalegezwe kidogo."

Mkulima kutoka Kijiji cha Mwenga Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Saidi Bomani alisema wakulima wanachangia pato la taifa kupitia mazao mbalimbali, hivyo ipo haja taasisi hizo kutambua mchango wao kwa maendeleo ya nchi.

"Taasisi za kifedha walione kundi hili la wakulima kama kundi muhimu, zielekeze mitaji yao kwetu sisi wakulima wa korosho na hata mazao mengine, badala ya kuelekeza tu kwa baadhi ya makundi na kuwaacha mkulima wakihangaika wakati ndiyo wanaochangia sehemu kubwa ya pato la taifa," alisema.

Ofisa Kilimo katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Ramadhani Sekija, alisema wamepokea malalamiko hayo na watayafanyia kazi kwa kushirikiana na taasisi nyingine za fedha.

Chanzo: HabariLeo