0

Wakulima wa chai kuhamasishwa viwanda vidogo

Wakulima wa chai kuhamasishwa viwanda vidogo

Mon, 22 Feb 2021 Source: HabariLeo

SERIKALI imesema itaendelea kuhamasisha wakulima wadogo kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata majani mabichi ya chai ili kusaidiana na viwanda vikubwa kumaliza upotevu wa majani hayo.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungumza na viongozi wa vyama 41 vya chai waliokusanyika mkoani hapa kuzungumzia changamoto za uchakataji chai yote inayozalishwa nchini inayofikia tani 37,000 kwa mwaka.

Bashe alisema, kwa sasa majani mabichi ya chai yamekuwa yakipotea bila kuchakatwa kutokana na viwanda vikubwa kutokuwa na uwezo wa kuchakata chai yote.

Alisema kutokana na uzalishaji wa chai kuwa mkubwa kuliko uwezo wa viwanda, atazungumza na Taasisi ya Agro-Connect inaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) badala ya kujenga kiwanda kutengeneza chai (blending) basi kijengwe kiwanda kwa ajili ya kuchakata (Processing) chai ili kupunguza adha ya chai kubaki shambani.

Alisema kuhusu katika changamoto ya barabara kuwa mbaya na hivyo kuchelewesha majani mabichi kufika kiwandani, Bashe alisema Taasisi ya Agro-Connect inakusudia katika mradi wake wa kusaidia wakulima, kutumia Euro milioni 48 kwa ajili ya kutengeneza barabara kutoka kwenye mashamba hadi kwenye masoko.

Aidha Serikali itaanzisha mnada wa chai nchini ili kusaidia wakulima wengi kupata soko la zao hilo hapa hapa nchini badala ya utaratibu wa sasa wa chaui ya Tanzania kupelekwa katika mnada unafanyika Mombasa,Kenya.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Nchini, Nicholaus Mauya alisema katika kuondoa changamoto hiyo, wakulima wadogo katika maeneo yote wanayolima chai yakiwemo ya Nyanda za Juu Kusini Mufundi, Njombe na Rungwe wanahamasishwa kuanzisha viwanda vidogo kwa ajili ya kuchukua majani ya chai mabichi yanayobaki baada ya viwanda kushindwa kutokana na uwezo mdogo.

Mauya alisema changamoto zilizopo katika sekta hiyo zikiondolewa kuna uwezekano mkubwa uzalishaji wa zao hilo wa kuongezeka kutoka tani 37,000 hadi tani 60,000 msimu wa 2024/25.

Chanzo: HabariLeo