0

Wafanyabiashara wadogo watakavyonufaika bomba la mafuta

Wafanyabiashara wadogo watakavyonufaika bomba la mafuta

Tue, 23 Feb 2021 Source: HabariLeo

WAFANYABIASHARA wadogo pembezoni mwa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) katika nchi za Tanzania na Uganda wataanza kunufaika na mradi huo kwa kujengewa uwezo, huku wenye mitaji midogo wakiongezewa mitaji.

Wakati Uganda ikiwa tayari imeshapokea dola za Marekani 500,000 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kwa ajili ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara wadogo na kati, majadiliano kwa Tanzania na benki hiyo yanaendelea vema ili nayo kupata fedha hizo.

Ujenzi wa bomba hilo la mafuta utagharimu Dola za Marekani bilion 3.55 na litakuwa na urefu wa kilometa 1,445, ambapo litasafirisha mapipa 200,000 hadi 216,000 ya mafuta ghafi kwa siku na kilometa kilometa 1,149 za bomba hilo zitajengwa ndani ya ardhi ya Tanzania.

Tanzania na Uganda zimewasiliana na benki hiyo kwa ajili ya kusaidia kufikia lengo hilo na nchi hizo mbili zilifanya kazi kwa pamoja kwa kuzingatia mkataba uliotiwa mwaka 2017.

Makubaliano hayo yanawezesha nchi hizo mbili kushirikiana katika maendeleo ya mradi huo.

Nchi hizo mbili zinataka kujenga uwezo wa jamii zilizo karibu na njia ya bomba hilo ili kuhakikisha zinanufaika na fursa hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Emmanuel Mugunga amesema mradi huo unatafuta kusaidia ukuaji wa pamoja wa sekta binafsi na uundaji wa takribani ajira 500 kando ya njia ya bomba hilo.

Akizungumzia upande wa Tanzania, Mratibu wa mradi wa bomba hilo kutoka Wizara ya Nishati Tanzania, Kisamarwa Nyangau alisema Uganda ilitangulia kidogo kufanya mchakato huo wakati ikiendelea na mazungumzo na benki hiyo.

Alisema majadiliano hayo yanafanyika kwa kufuata miongozo ya serikali na kiasi kamili cha fedha kitakachotolewa na idadi ya wanufaika itajulikana baada ya kumaliza majadiliano hayo.

“Majadiliano yakikamilika baina ya serikali na benki hiyo taarifa rasmi zitatolewa kuhusu programu hiyo kwa wajasiliamali walio pembezoni mwa bomba hilo,” alisema.

Chanzo: HabariLeo