0

Wadau wa nyuki wataka wawekezaji wa viwanda

Wadau wa nyuki wataka wawekezaji wa viwanda

Thu, 25 Feb 2021 Source: HabariLeo

WADAU wa sekta ya nyuki nchini, wameiomba serikali iwaunganishe zaidi na washirika wa maendeleo ili kutumia fursa zilizopo kutangaza na kukuza soko la asali ya Tanzania kimataifa na kuinua uwekezaji wa viwanda nchini.

Walisema hayo kwa nyakati tofauti jana katika siku ya pili ya Kongamano la Kimataifa la Sayansi juu ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu na Nyuki kwa Maisha Endelevu na Uchumi wa Viwanda.

Kongamano hilo lilifunguliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro kwa niaba ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Jana wadau wa ufugaji nyuki waliishukuru serikali kwa namna inavyohamasisha ufugaji nyuki kibiashara na kuiomba iwaunganishe zaidi na washirika wa maendeleo wa nchi mbalimbali ili kupanua uelewa, ubunifu na ujuzi kwa lengo la kupata masoko zaidi na uwekezaji wa viwanda vingi zaidi nchini.

Kwa mujibu wa Dk Ndumbaro, kuna viwanda 21 vya nyuki nchini na vitano vinatarajiwa kukamilika hivi karibuni. Alisema lengo la serikali ni kuwa na viwanda zaidi ya 200 vidogo kwa sekta ya nyuki ikimaanisha kila halmashauri iwe na kiwanda.

Mratibu wa Kikundi cha Umoja kutoka Kijiji cha Mbatamila wilayani Tunduru, Michael William, aliishukuru serikali kwa kuwashika mkono kwa kuweka mazingira yaliyowawezesha kuanzisha kikundi hicho na kuomba kuwaunganisha na mitandao ya sekta ya nyuki kimataifa.

Katibu wa Kikundi cha Umoja, Yassin Musa aliiomba serikali kuwapatia vifaa maofisa ugani wa halmashauri , kama vile pikipiki ili wawafikie wafugaji wa nyuki na kuongeza ufanisi, elimu na ubora wa mazao ya nyuki.

Kuthibitisha hilo, Ofisa Ufugaji Nyuki Wilaya ya Bukombe, inayoongoza kwa kuzalisha asali kwa wingi mkoani Geita, Dafrosa Shayo, alisema ni kweli serikali imejitahidi kuwainua wafugaji wa nyuki kwa kuwaunganisha kupitia vikundi, lakini wao wanakabiliwa na uhaba wa vitendea kazi na watumishi.

"Kwa mfano Juni mwaka huu tutaanzisha kiwanda cha asali, lakini ili uzalishaji uwe mkubwa na kwa ubora unaotakiwa kimataifa, lazima vitendea kazi viboreshwe na watumishi waongezwe ili tuwafikie wadau wengi zaidi vijijini," alishauri Shayo.

Kongamano hilo la siku tatu, linamalizika leo ambapo litatoa maazimio ya namna ya kukabiliana na changamoto zinazoikumbuka sekta ya misitu na nyuki katika mnyororo wa thamani wa mazao ya sekta hiyo, sera na sheria.

Chanzo: HabariLeo