0

Viongozi watakiwa kutumia bidhaa za ngozi za ndani

Viongozi watakiwa kutumia bidhaa za ngozi za ndani

Fri, 23 Oct 2020 Source: HabariLeo

RAIS John Magufuli amewataka viongozi wakuu wa vyombo vya dola, mawaziri, viongozi wengine wa serikali na madhehebu ya dini, kujiandaa kutumia bidhaa za ngozi zinazozalishwa hapa nchini ili kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kwa kuagiza nje ya nchi.

Tanzania kwa sasa inaagiza zaidi ya jozi milioni 52 za viatu kutoka nje ya nchi na hivyo kutumia kiwango kikubwa cha fedha za kigeni, jambo ambalo linaweza kuepukika na fedha hizo kutumika kwenye mambo mengine ya maendeleo.

“Nimeangalia viatu walivyovaa mawaziri Jenista Mhagama na George Simbachawene, Nikaangalia changu mwenyewe, mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, viongozi wa dini na watu wengine, nimegundua tuna kazi ya kufanya maana wote tumevaa viatu kutoka nje ya nchi,” alisema.

Rais Magufuli alisema hayo wakati akifungua Kiwanda cha ngozi kinachomilikiwa na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa asilimia 86 kwa ubia na Jeshi la Magereza lenye asilimia 14.

Kiwanda hicho kinatoa ajira zaidi ya 3,000. “Pamoja na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, lakini pia ufunguzi wa kiwanda cha Kilimanjaro International Leather Industries cha mjini Moshi, utaongeza soko la bidhaa za ngozi nchini sanjari na kuwahikikishia wafugaji uhakika wa soko”alisema.

Chanzo: HabariLeo