0

Uvunaji shirikishi wa misitu

Uvunaji shirikishi wa misitu

Mon, 16 Nov 2020 Source: HabariLeo

JE, kuna uhusiano wowote wa maendeleo ya jamii fulani na suala zima la ushiriki sawa wa wanawake na makundi mengine ya pembezoni katika shughuli za maendeleo?

Na je, miradi mbalimbali ya maendeleo inayoanzishwa nchini mwetu, iwe imeanzishwa na serikali au na taasisi binafsi imekuwa ikizingatia suala zima la usawa wa kijinsia, kwa maana ya kuona kunakuwa na uwiano sawa wa ushiriki wa makundi yote ya kijamii?

Makala haya, yanajaribu kujibu maswali hayo. Katika kujibu swali la kwanza la uhusiano wa maendeleo ya jamii na usawa wa kijinsia, Profesa John Jeckoniah kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo anasema: “Ukosefu wa usawa wa kijinsia katika jamii yoyote ile hauathiri tu watu binafsi bali unaweza kubadilisha uchumi mzima wa jamii.”

Akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu Jinsia na Usimamizi Shirikishi wa Msitu ya Jamii na Mnyororo wa Thamani wa Bidhaa za Misitu, anasema: “Usawa wa kijinsia siyo haki ya kimsingi tu ya binadamu, lakini ni jambo la lazima katika kuwa na dunia yenye amani na ustawi.”

Anaongeza kwamba kimsingi, upendeleo au unyanyasaji wa kijinsia mara nyingi unafanyika bila jamii kuelewa kwamba huu ni unyanyasaji kutokana na kuwa sehemu ya mila, tamaduni, imani za kidini au mazoea ya jamii husika.

Miradi ya maendeleo Shirila la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), walianzisha Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa nchini (TTCS) maarufu kama “mkaa endelevu” kwa njia ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ).

Msingi wa mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC) unatokana na ukweli kwamba, kwa miongo kadhaa Watanzania wataendelea kutumia mkaa na kuni kwa ajili ya kupikia kutokana na mazingira yanayozunguka nishati zingine mbadala.

Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba asilimia 96 ya kaya hapa nchini zinatumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia. Asilimia 88.2 ya kaya katika jiji la Dar es Salaam na asilimia 79.3 katika miji mingine zinatumia mkaa kwa kupikia (kwa mujibu wa NBS, 2016 EASR).

Lakini tatizo ambalo lipo ni uvunaji wa mkaa katika misitu mingi ya vijiji kufanywa kiholela na hivyo kuchagia katika uharibifu wa misitu.

Uholela huo huchangia kati ya asilimia 10 na 30 ya uharibifu wa misitu nchini huku asilimia kubwa iliyobaki ikisababishwa na kilimo, hasa cha kuhama hama.

Takwimu zinaonesha kwamba tani milioni 2.3 za mkaa zinatumika kwa mwaka hapa nchini na kwamba mchango wa sekta ya mkaa kwenye uchumi wa nchi ni takribani Sh trilioni 2.2.

Hakuna zao lolote katika mazao makubwa ya biashara kama vile korosho, kahawa na pamba linaloingiza kiasi hicho cha fedha. Hata hivyo, mapato yanayopotea kwa mwaka kutokana na mkaa kuzalishwa holela bila usimamizi yanafikia shilingi bilioni 220.

Vijiji takribani 30 katika wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro ndivyo vilivyoteuliwa kama vijiji vya mfano katika kutekeleza mradi huo.

Uvunaji wa mkaa kwa njia endelevu uliendana na vijiji kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi, kuanzisha kamati za ulinzi wa raslimali za misitu, kuanzisha kilimo hifadhi, uvunaji wa mbao, ufugaji wa nyuki na kuanzishwa kwa vikundi vya kuweka na kukopa.

Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba vijiji vinavyoendesha mradi huo vimekuwa vikipata mamilioni ya pesa yanayotokana na raslimali misitu.

Huku halmashauri pia zikinufaika, vijiji vingi vya mradi vinatumia pesa za mapato kuimarisha ulinzi wa misitu, kujenga shule na madarasa, kuchimba visima vya maji, kulipia wananchi bima na huduma zingine za kijamii, mambo ambayo yalipaswa kutoka kwenye bajeti za halmashauri za wilaya au serikali kuu.

Kwa mfano, katika kijiji cha Ulaya Mbuyuni, kilichoko Kilosa mkoani Morogoro, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Selemani Hashimu, anasema: “Kabla hatujaanza mradi, kijiji kilikuwa hakiingizi mapato yoyote na tulikuwa tegemezi kwa serikali au kuwachangisha wanakijiji tunapokuwa na mradi wa maendeleo.

Lakini kupitia misitu sasa tunatekeleza miradi mbalimbali ya kijamii kwa fedha zetu.” Anasema kabla ya mradi kulikuwa na wavamizi wengi katika msitu wa kijiji lakini kupitia elimu wameondoka na kwamba baada ya wananchi kuona faida za misitu yao, wamekuwa walinzi namba moja wa misitu kwani sasa hawaioni kama mali ya serikali.

Anasema kupitia ushuru wanaopata kutokana na uvunaji wa msitu wamekuwa wakiingiza wastani wa shilingi milioni 100 kwa mwaka. Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, mbali na faida za kipesa kwa kijiji, wachoma mkaa wakiwemo wanawake wamepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto, kujenga nyumba au kuanzisha miradi mingine ya kilimo.

Mradi mpya Kutokana na mafanikio hayo, TFCG na Mjumita kwa udhamini wa SDC wameanzisha Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Misitu (CoFoREST).

Huu ni mwendelezo wa mradi wa TTCS lakini unaojengea jamii uwezo katika kutumia mafanikio yaliyopatikana katika vijiji 30 ili yabaki kuwa endelevu huku vijiji vingine pia vikianzisha miradi kama hiyo.

Je, makundi yote ya kijinsia, wanaume, wanawake, vijana, walemevu na mengine ya pembezoni (disadvantaged groups) yanafaidika sawa na shughuli nzima ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii kupitia shughuli za kibiashara zinazotokana na raslimali misitu?

Ni katika muktadha huo, TFCG na MJUMITA waliamua kukipa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) jukumu la kufanya utafiti, ili kujua hali halisi na namna nzuri ya mradi mpya kujumuisha masuala ya kijinsia.

Watafiti walitembelea vijiji 10 kati ya 30 vinavyotekeleza mradi katika wilaya za Morogoro, Kilosa na Mvomero na tayari wametoa ripoti yao ya awali. Ushiriki wa wanawake waongezeka Katika utafiti wao, Profesa Jeckoniah na mwenzake Profesa Suzana Augustino kutoka SUA wamegundua kwamba mradi wa TTCS umesaidia sana kuongeza ushiriki wa wanawake katika kuvuna raslimali za misitu kibiashara na kwa njia endelevu.

Profesa Suzana anasema wanawake katika vijiji vya mradi sasa wanavuna mkaa, kazi iliyoonekana huko nyuma kuwa ya wanaume na wengi wanakiri sasa kujipatia pesa kutokana na mkaa.

Lakini anasema tofauti na wanaume, bado wanawake wanaovuna mkaa wanawategemea wanaume kwa kuwakatia miti na kuwapangia matanuri kwa kuwalipa pesa.

Pia anasema wengi bado hawajajiingiza kwenye ukataji wa mbao unaondelea kuonekana kama kazi ya wanaume, hali inayochangiwa pia na wanawake wengi kukosa utalaamu wa kupasua mbao.

Katika wasilisho la utafiti wao kwa wadau mbalimbali wa misitu wakiwemo waandishi wa habari, maprofesa hao wanasema, hata hivyo, kwamba bado kuna wananchi wachache ambao hawaoni kama uchomaji mkaa ni shughuli inayomfaa mwanamke na kuna wachache ambao waume zao hawajaridhia kabisa wake zao kushiriki katika shughuli ya uvunaji mkaa.

Profesa Suzana anasema kitu kikubwa ambacho wanawake wengi katika vijiji vya mradi wanashiriki na kimewapa manufaa makubwa ni benki za kuweka na kukopa.

Hata hivyo, anasema bado wanaume wengi hawajajiunga na benki hizo za vijijini na kunufaika nazo kutokana na kusumbuliwa mtazamo usio sahihi kwamba vicoba ni mambo ya wanawake!

Anasema wanawake wengi katika maeneo ya miradi, wameongeza pia uelewa kuhusu haki zao huku nguvu za kiuchumi wanazoendelea kupata zikiwafanya wajiamini zaidi na kutaka uwakilishi kwenye mabaraza ya maamuzi uwe wa 50 kwa 50.

Wanawake na kazi nyingi Watafiti hao wanasema kwamba licha ya idadi ya wanawake kuongezeka katika shughuli ambazo awali zilionekana kama za wanaume kumeibuka tatizo la wanawake kujikuta wanafanya kazi nyingi kwani pamoja na kushughulika katika kuzalisha, kazi za nyumbani bado zinawasubiri wao.

Kazi hizo ni kama kupika, kulea watoto, kuhudumia wagonjwa na wazee, kuchota maji na nyingine kama hizo.

“Muda ni rasilimali muhimu sana. Katika utafiti wetu tumeona mwanamke anaposhiriki katika shughuli za uzalishaji kama kuchoma mkaa, anaongeza majukumu na muda kuwa finyu kwani anapokuwa kwenye kuzalisha mali, majukumu yake ya nyumbani huwa bado yanamsubiri,” anasema Profesa Jeckoniah.

Inapendekezwa kwamba kwa sababu mwanamke anapokuwa anashughulika katika kazi za kuongeza kipato ni kwa faida ya familia pia, ni wakati sasa wa wanaume kubadilika na kusaidiana na wake zao katika shughuli nyingine za nyumbani kama kupika, kufua na kulea watoto.

Profesa Jeckoniah anasema kwamba kimsingi hakuna kazi ambayo ni kwa ajili ya mwanamke na nyingine za mwanaume na kwamba mgawanyo huu unatokana na mitazamo ya kimazoea, mila na tamaduni kwani mwanaume akifanya kazi hizo hapungukiwi na chochote katika uwanaume wake.

“Kazi maalumu ambazo mwanaume hawezi kifanya ni kuzaa na kunyonyesha na kazi ambayo mwanamke hawezi kufanya ni kutia mimba, basi,” anasema.

Watafiti hao, hata hivyo, wanasema bado wanaume wengi wanaonekana wagumu kubadilisha mitazamo na mazoea kwa wanawake. “Kinachoonekana ni kwamba wanaume hawataki mabadiliko katika masuala yanayobebwa na mila na desturi kwa kuwa yanawanufaisha wao,” anasema Profesa.

Itaendelea

Chanzo: HabariLeo