0

Ujio mashine ya kisasa kupaisha kilimo cha dengu

Ujio mashine ya kisasa kupaisha kilimo cha dengu

Tue, 6 Oct 2020 Source: HabariLeo

WAKULIMA wa zao la dengu wilayani Shinyanga wanaelekea kuondokana na njia za kienyeji au kilimo cha mazoea katika kuandaa mashamba yao, kuvuna hadi kupepeta.

Inaelezwa kwamba kilimo cha mazoea kilikuwa kikiwafanya watumie nguvu nyingi, watu wengi na muda mwingi lakini ubora wa mazao yao sokoni ukiwa chini kujikuta bei ikishuka pia.

Wakulima Juliana Mhongela na Kulwa Sadiki wanapozungumzia eneo la upepetaji wa dengu kwa mkono, wanasema hali hiyo ilikuwa ikiwafanya wakohoe au kuugua mafua kutokana na vumbi huku wakitumia muda mwingi kujaza gunia moja la dengu.

Theresia Ligwa mkazi wa kijiji cha Muongozo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga anasema yeye amekuwa akifanya vibarua vya kupepeta dengu na kuondoa maganda na kujipatia fedha kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya familia yake.

Hata hivyo, anasema changamoto ambayo amekuwa akikumbana nayo ni kikohozi na mafua kutokana na vumbi. Yacob Kilasa na Hellen Makwaya ambao ni wakulima wa dengu wanasema wamekuwa wakilima zao hilo kwa kupata changamoto tangu kuanza kuandaa shamba na kupanda.

Wanataja changamoto hizo kuwa ni kutumia muda mwingi katika kubanjua maganda na kisha kupepeta dengu.

Ujio wa mashine inayoitwa multi-plant inaelezwa kwamba ni moja ya hatua muhimu katika kuandaa shamba la dengu, uvunaji na uandaaji wa dengu kutokana na kurahisisha kazi.

Halikadhalika, inaelezwa kwamba hatua hiyo itasababisha dengu kupelekwa sokoni zikiwa kwenye ubora kuliko zinapoandaliwa na kupepetwa kwa mikoani na huenda hatua hiyo ikasaidia kupandisha bei ya zao hilo pia.

Yuda Jacob, mkazi wa kijiji cha Muongozo aliyenunua mashine ya inayokwenda na teknolojia ambayo kwa wakati mmoja ina banjua maganda, inapepeta, inafanya kazi ya kupanda kwa kunyoosha mstari na kuweka mbolea anasema kuwa atatumia mashine hiyo kwa kukodisha wakulima wenzake ili kuwarahisishia kazi na yeye mwenyewe kuitumia kwenye shughuli zake za kilimo.

Athony Charles, mfanyabiashara wa dengu kutoka mkoani Mwanza anasema kuwa wamefurahi kusikia uwepo wa mashine hiyo ambayo itakuwa ikichakata zao hilo na kuboresha ubora wake.

Anasema hatua ya kutumia trekta katika kukanyanga dengu ilikuwa inasababisha kuzifanya ziwe chafu na mchanga mwingi, hali iliyokuwa inachangia bei yake kuporomoka kwenye soko.

Charles anasema wakulima wa zao la dengu wamekuwa wakitumia njia ya kukanyaga na trekta na kisha kuweka chini wakati wa kupepeta wakilazimika kutumia muda mwingi kusubiri upepo ndipo waweze kuondoa maganda.

Kwiyolecha Kilijiwa, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Msingi (Amcos) kutoka kijiji cha Muongozo, kata ya Mwenge katika halmashauri hiyo ya wilaya ya Shinyanga anasema utumiaji wa mashine, siyo tu kwamba utaboresha bali pia kurahisisha kazi kwa mkulima wa dengu.

Kilijiwa anafafanua kwamba kwa kilimo cha mazoea kisichotumia teknolojia wakulima huanzia kwa kumwaga mbolea kwa mikono, kupanda, kuvuna na lakini kubanjua maganda kwa kutumia trekta ambalo hufanya kazi ya kukanyanga dengu lakini njia hiyo ikipoteza thamani ya ubora wa dengu.

“Kwa kufanyiwa majaribio kwa zao la dengu namna ya kubanjua maganda, mashine hii imeonekana ni nzuri kwani haivunji punje za dengu na kumsababishia mkulima hasara katika soko,” anasema Kilijiwa.

Kilijiwa anasema utumiaji wa mashine utarahisisha kazi ya kupepeta ambayo mara nyingi imekuwa ikifanywa na wanawake baada ya trekta kukanyaga dengu hizo.

Pia ni hatua itakayowaepusha kupata magonjwa katika mfumo wa upumuaji, ikiwa ni pamoja na mafua na kikohozi.

Kutokana na kutokuwa na utaratibu wa stakabadhi ghalani, bado wakulima wamekuwa wakilazimika kuuza dengu yao kwa makampuni binafsi na walanguzi.

Kilijiwa anasema wizara ya kilimo ilitangaza kuwa zao la dengu, choroko na mpunga yatanunuliwa na vyama vya ushirika kwa mfumo wa stakabadhi ghalani lakini bado hilo halijafanyika na kwamba kwa sasa kilo moja ya dengu inanunuliwa kwa shilingi 800 lakini kupitia Amcos bei hufika shilingi 1,010 kwa kilo na kwamba bado bei siyo elekezi.

Christina Mabula, ofisa masoko kutoka kampuni ya Agricom inayojihusisha na zana za kisasa za kilimo anasema kuwa wamekuja kuonesha mashine hiyo ya Multi-crop plant kwa wakulima kwa kuwa inarahisisha kazi.

Anasema inasaidia kulainisha udongo, pale mkulima anapokuwa anaandaa shamba na inasaidia kupanda mazao ya aina mbalimbali ya mfumo wa mbegu.

Mabula anasema wakulima bado wanalima kwa kutumia teknolojia ya zamani, lakini sasa wanashauriwa kubadilika ili kuweza kuokoa muda na kunufaika na kilimo chao.

“Wengi wanatumia nguvu kubwa lakini wanaishia kupata mazao kidogo lakini mashine inawarahisishia kazi kama vile kulainisha udongo katika uandaaji shamba, kuvuna, kupiga na kupepeta.

“Mashine hii inaongeza kipato kwa wakulima kwani ukiwa nayo, hutumia saa moja kubanjua magunia 40 huku ikipepeta moja kwa moja na siku moja huweza kubanjua magunia 320,” anasema.

Anasema mashine hiyo inapunguza idadi kubwa ya watu wanaoshiriki katika kuzalisha dengu hadi kuiandaa kwa ajili ya soko.

Mabula anawashauri wakulima wanunue zana bora za kilimo zinazokwenda kisasa na zinazosaidia kuongeza thamani ya mazao yao.

Mtaalamu wa kufundisha matumizi ya mashine hizo kutoka Kanda ya Ziwa, Musa Somon, anasema, mbali na dengu mashine hiyo inatumika pia kwenye zao la dengu, mpunga na choroko.

Chanzo: HabariLeo