0

Uchumi wa kilimo cha maharage unavyopelekwa Kusini

Tue, 13 Oct 2020 Source: habarileo.co.tz

MAHARAGE ni zao maarufu zaidi duniani kati ya mazao mengine ya jamii ya mikunde.

Sehemu kubwa ya Afrika Mashariki, maharage yanazalishwa kwa matumizi ya nyumbani na kwa ajili ya kuuza.

Mwaka 2013 Tanzania ilikuwa nchi ya sita katika uzalishaji wa maharage makavu duniani. Kwa mwaka huo Tanzania ilizalisha tani 1,150,000.

Nchi ya kwanza kwa takwimu za mwaka huo kwa uzalishaji wa maharage makavu duniani ilikuwa ni Myanmar (tani 3,800,000), ikifuatiwa na India (tani 3,630,000), Brazil (tani 2,936,444), China (tani 1,400,000) na Mexico (tani 1,294,634).

Tanzania kwa mwaka huo ilizitangulia nchi za Marekani (tani 1,110,668), Kenya (tani 529,265), Uganda (tani 461,000) na Rwanda (tani 438,236).

Wakulima wa Afrika Mashariki wanazalisha zaidi ya nusu ya maharage yote yanayozalishwa barani Afrika.

Nchini Tanzania, mara nyingi maharage yanapandwa pamoja na mahindi au na zao la kudumu kama ndizi au kahawa.

Pamoja na umaarufu huo wa Tanzania, mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) imekuwa mikoa migeni ya kufanya kilimo cha maharage kinachoeleweka.

Wakulima wa mikoa hiyo ya kusini wamezoea kulima ufuta, korosho, choroko, mbaazi, na kwa kiasi fulani maharage kwa kubahatisha.

Wataalamu wa Taasisi ya Utafuti wa Kilimo Tanzania (TARI), kituo cha Naliendele, baada ya kuona kuna wakulima katika mikoa ya Lindi na Mtwara wameanza kujishughulisha na kilimo cha maharage waliamua kufanya utafiti wa mbegu zinazofaa kwa maeneo hayo.

Lengo la kushauri matumizi bora ya mbegu na kilimo chenye tija.

Katika utafiti wa kilimo kisichotegemea maji ya kumwagilia wataalamu hao walilenga kupata maeneo ambayo yana ardhi inayofaa kwa kilimo cha maharage kwa kuzingatia mwinuko wake kutoka usawa wa bahari.

Mwinuko unaofaa kwa maharage mara nyingi ni kuanzia mita 700 mpaka 900 kutoka usawa wa bahari katika ukanda huu wa kusini.

Kwa mujibu wa mtafiti, Dk John Tenga wa Tari- Naliendele, kazi ya utafiti ilianzia kwa kutathmini kilimo cha maharage ambacho wakulima katika maeneo hayo walikuwa wakilima kama mboga.

Kwa kuuona uhitaji wa maharage kama mboga na pia kibiashara kwa wakulima wa maeneo hayo ndipo kituo cha utafiti Naliendele kwa kushirikiana na kituo cha utafiti Uyole na kwa kipitia taarifa mbalimbali za kiutafiti, wakateua mbegu bora zinazofaa kwa mikoa ya Kusini.

Kwa mujibu wa Dk Tenga, mbegu ambazo walizichukua kwa ajili ya utafiti ili kuona ubora wake kwa maeneo waliyoyachagua zilikuwa ni za aina 11 ambazo bado ziko katika utafiti lakini aina tatu ambazo zimepatishwa hadui sasa Pasi, Rosenda na Fibea.

"Kiukweli kilimo cha maharage ni kipya katika maeneo hayo. Hapo zamani mazao ambayo wakulima walizoea kulima ni karanga, njugu na mbaazi," anasema Dk Tenga na kuongeza kwaba kwa upande wao wameshakamilisha utafiti na sasa kuanzia mwaka huu wanawaelekeza wakulima ili waanze kuona matokeo ya maelekezo yao.

"Jambo linalohitajika kukuza zao hili la maharage kuwa zao la biashara ni kufuata kanuni za Kilimo Bora cha maharage. Pili ni kwa wakulima kulima kwa wingi ili upatikanaji wake usiwe haba hivyo kuchochea biashara ya maharage katika ukanda huo wa Kusini,” anasema Dk Tenga.

Anasema soko lipo wazi ukizingatia kuwa maharage ndiyo mlo wenye protini unaotegemewa na kaya kwa zaidi ya asilimia 75.

“Maharage ya Lindi na Mtwara yatakuwa na soko kubwa kwa kuwa katika utafiti yameonekana kukomaa mapema zaidi kabla ya mavuno yanayofanyika Nyanda za Juu Kusini kwenye mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Iringa,” anasema.

Utafiti uliofanywa na Tari Naliendele anasema ulilenga kuwapatia mbegu ambayo inapambana na wadudu na magonjwa yakiwemo magonjwa yanayosababishwa na fangasi, virusi na bakajani.

Anasema mbegu iliyofanyiwa kazi iliangaliwa kwa uhakika wa hali ya hewa pamoja na kuvumilia ukame.

Katika upandaji wa maharage msimu huu anasema kulikuwa na mvua kidogo na watu walichelewa kuanza kilimo lakini bado walivuna.

Dk Tenga anasema baada ya kuona kwamba kuna maeneo yenye uwezo wa kuzalisha maharage yenye ubaridi kidogo yakiwa katika usawa wa mita 700 mpaka 900 toka usawa wa bahari wameanza ushawishi ulimaji wa maharage kibiashara.

Maeneo ya Chilangala katika mkoa wa Mtwara pamoja na Rondo katika mkoa wa Lindi ni maeneo ambayo yanakidhi vigezo vya kulimwa maharage yakiwa katika mwinuko kati ya mita 800-900 kutoka usawa bahari.

Katika maeneo hayo maharagwe yanachukua muda mfupi zaidi kwa mbegu zilizofanywa utafiti.

"Tumepeleka mbegu 11 za utafiti na tatu zilizokuwa tayari na tumeona kwamba mbegu hizi zinafaa," anasema Dk Tenga.

Anasema kwamba kilimo hicho kimeonesha kwamba wakulima wanaweza kuvuna tani 2.5 mpaka tatu kwa hekta moja, na kwamba kwa mikoa hiyo miwili maharage yanakomaa mapema na hata kama mvua ni kidogo.

Mwenyekiti mstaafu wa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, Ahmaid Makoroganya, anasema kwamba kilimo hicho kikishika kasi kitasaidia sana wananchi wa mikoa hiyo kwa kuwa kwa sasa wanafuata maharage mikoa ya Mbeya na Ruvuma na kuuza bidhaa hiyo kwa Sh 2,500 hadi Sh 3,000 kwa kilo kwa bei ya rejareja.

"Majaribio yanaonesha mafanikio makubwa, wawekezaji waje kusaidia kuinua kilimo hiki," anasema Makoroganya.

Violet Richard ambaye ni Ofisa Kilimo katika Halmashauri ya Mtama anashukuru kuwapo kwa msukumo huo wa kilimo cha maharage kutokana na utafiti uliofanywa na Tari Naliendele na kwamba wanapenda kushirikiana na taasisi hiyo ili kunyanyua zao hilo jipya.

Mkulima Somoe Blazichochote anasema kwamba wamebaini kwamba kuna jambo jema sana katika mbegu za maharage kutoka Naliendele kwa kuwa katika majaribio walipewa kilo tisa za mbegu kwa ajili ya majaribio na wamevuna kila 69 za maharage kutokana na kilo hizo tisa.

Naye Jabir Mkapunda wa kijiji cha Mkopi anasema kilimo cha maharage kilichoanza kufanyiwa kazi miaka miwili iliyopita sasa kimekuwa na nguvu zaidi kwa kupanda mbegu toka Naliendele ambazo zimeonesha kufanya vyema katika maeneo yaliyochaguliwa.

Wakulima wengine Zaituni Mohamed na Halima Mwinyege wanasema kwamba wanaona hatima njema ya kilimo cha maharage kutokana na uwepo wa mbegu bora na pia kuelekezwa kilimobiashara kinachofaa kwa mikoa hiyo.

Kituo cha Utafiti cha Naliendele kiliendesha utafiti wa zao la maharage kutokana na ukweli pia kuwa mikoa hiyo iko pia karibu na soko la Dar es Salaam lakini pia kutoa soko la kwa wananchi wa mikoa hiyo ili kujipatia protini kwa urahisi.

Ukiangalia mwaka huu hadi Mei mathalani, bei ya kilo moja ya maharage imeendelea kubaki Sh 2,500 kwa kilo kwa mlaji bei ambayo inahakikisha uwapo wa soko lisiloyumba la zao hilo, mikoa hiyo ya Kusini.

Ukitazama masoko mengine unaona dhahiri kwamba kwa muda zao hili ambalo lina matumizi makubwa miongoni mwa kaya nyingi nchini limekuwa na bei ya wastani katika masoko makubwa ambayo ni Dar es Salaam, Morogoro na Mara.

Soko la Dar es Salaam na Morogoro bei zake kwa Machi mwaka huu zilikuwa zinapendeza kwa mkulima.

Machi 4, 2020 bei ya juu kabisa ya zao la maharage ilishuhudiwa katika masoko ya mkoa wa Morogoro ambapo gunia la kilo 100 liliuzwa kwa Sh 265,000.

Bei ya maharage ya gunia la kilo 100 katika soko la Kinondoni jijini Dar es Salaam ilikuwa inauzwa Sh 260,000 na bei ya chini ilikuwa ya mkoa wa Mara ya Sh 100,000.

Kwa mujibu wa takwimu za bei za jumla za mazao makuu ya chakula nchini zilizotolewa Machi 4, 2020 na Wizara ya Viwanda na Biashara, zilionyesha kuwa bei ya maharage ya gunia la kilo 100 inauzwa Sh 260,000 katika soko la Kinondoni jijini Dar es Salaam ikiwa imeshuka kutoka Sh 280,000 iliyorekodiwa nyuma yake jijini humo.

Maharage ni moja ya chakula ambacho kina protini nyingi na ndio mboga ya 'serikali' kutokana na kuwapo katika matumizi ya watu wengi wa hali ya kawaida.

Kazi ya protini ni kujenga mwili na kuwezesha ukuaji wa mwili hasa kwa watoto na pia husaidia kutengeneza kinga ya mwili.

Ofisa Kilimo wilaya ya Newala, Alford Mpanda akizungumza kuhusu juhudi za Tari Naliendele anasema kwamba ni msaada mkubwa katika kuhakikisha kwamba wananchi wanaongeza zao lingine la biashara na kujinyanyua kiuchumi lakini pia wanapata lishe bora.

Chanzo: habarileo.co.tz