0

Tari yapongezwa kuwapatia mafunzo watalaamu wake

Tari yapongezwa kuwapatia mafunzo watalaamu wake

Wed, 18 Nov 2020 Source: HabariLeo

OFISA Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Yibarila Kamele amewapongeza wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele.

Pongezi hizo ni kwa kuwapatia mafunzo wataalamu wao wakiwemo maofisa ugani, wakulima ambao tayari wameshaanza kuzalisha korosho katika halmashauri hiyo pamoja na utoaji wa mbegu bora za korosho.

Kamele alitoa pongezi hizo wakati wa mafunzo ya siku mbili kwa wakulima wa zao hilo kuhusu kilimo bora cha zao la korosho na ubora wake, mafunzo ambayo yamefanyika kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga chini ya Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) kwa kushirikiana na TARI Naliendele.

Mafunzo hayo yana lengo la kuwapatia wakulima hao teknolojia mpya za kilimo bora cha zao la korosho kwa kupanda mbegu bora, kudhibiti wadudu waharibifu na magonjwa katika zao hilo ili ifikapo mwaka 2025 Tanzania iweze kufikisha tani milioni moja kwa mwaka kutoka tani 313,000 kwa sasa.

Alisema zao la korosho likiwa kama ni zao la kudumu na la kibiashara kwa halmashauri hiyo ilianza uwekezaji mwaka 2016/17 ambapo ilichukua sehemu ya mapato yake ikaweza kununua mbegu ya miche ya mikorosho, baadaye mwaka wa pili mbegu hizo walizigawa bure kwa wananchi, lengo likiwa ni kuwekeza zao hilo kwa wananchi ili wawe na zao la kiuchumi ambalo ni la kudumu.

Kwa upande wao, wataalamu kutoka Tari akiwemo Stella Mfune wakati akitoa mada kwa wakulima hao, alisema kupitia mafunzo yanayotolewa pamoja na mbegu zinazotolewa na taasisi hiyo zinawezesha wakulima kujenga uaminifu kutokana na mafanikio yake yanavyoanza kuonekana kwa haraka ikilinganishwa na zile mbegu za zamani walizokuwa wakizitumia.

Chanzo: HabariLeo