0

Tanzania yazalisha chanjo sita za mifugo

Tanzania yazalisha chanjo sita za mifugo

Tue, 6 Oct 2020 Source: HabariLeo

TANZANIA imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa chanjo za mifugo baada ya kuzalisha chanjo sita katika muda mfupi. Aidha, chanjo ya saba inatarajiwa kufanyiwa majaribio hivi karibuni baada ya kuwa majaribio ya awali yakiwa yameanza.

Hayo yamefahamika mwishoni mwa wiki mjini hapa wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo), Profesa Elisante ole Gabriel pamoja na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini katika taasisi mbili zinazohusika na chanjo za mifugo.

Taasisi hizo ni Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) na Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI). Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dk Furaha Mramba, tangu uzalishaji wa chanjo uanze rasmi mwaka 2014, wameshatengeneza chanjo sita.

Dk Mramba alisema TVI ilianza kwa kuzalisha chanjo moja tu dhidi ya ugonjwa wa mdondo wa kuku yenye jina la kibiashara la TEMEVAC.

Lakini alisema hadi kufikia mwaka huu, wanazalisha chanjo aina sita ambazo ni chanjo dhidi ya ugonjwa wa Mdondo kwa kuku; ya Kimeta kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo; ya Chambavu kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo, ya Kutupa Mimba kwa ng’ombe, na chanjo dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya Ng’ombe kwa ajili ya ng’ombe.

Aliitaja ya sita kuwa ni ya mchanganyiko wa Kimeta na Chambavu ya kukinga magonjwa hayo mawili kwa mara moja. “Lengo la karibuni la wakala ni kupanua wigo wa aina za chanjo zinazozalishwa kwa kuongeza chanjo tatu za kimkakati,” alisema Dk Mramba na kuzitaja chanjo hizo tatu ni ya Homa ya Mapafu ya Mbuzi (CCPP), Sotoka ya mbuzi (PPR) na Kichaa cha Mbwa (Rabies).

Kuhusu Homa ya Mapafu ya Mbuzi, alisema, “Majaribio ya awali ya chanjo dhidi ya Homa ya Mapafu ya Mbuzi tayari yameshaanza na inategemewa kuwa ifikapo Desemba 2020 chanjo hii itakuwa tayari inafanyiwa majaribio katika baadhi ya maeneo.”

Alisema kwa majaribio ya chanjo ya Sotoka ya mbuzi yanategemewa kuanza baada ya watumishi kupata mafunzo maalumu juu ya uzalishaji huo.

Dk Mramba alisema kwa ile ya Kichaa cha Mbwa majaribio ya utengenezaji wa Mbegu Kuu kutokana na vimelea vya virusi vya ugonjwa huo yanaendelea kufanywa na maabara ya CIDB.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Hezron Nonga alisema kuna magonjwa 13 ya kimkakati ambayo Tanzania inataka kuyadhibiti ili kuleta tija katika mifugo nchini.

Dk Nonga aliyataja kuwa ni homa ya mapafu ya ng’ombe, homa ya mapafu ya mbuzi, midomo na miguu, mapele ngozi, kutupa mimba, sotoka ya mbuzi na kondoo na ndigana kali, mdondo, kichaa cha mbwa, homa ya Bonde la Ufa, homa kali ya nguruwe na chambavu.

Alisema nia ya serikali ni kuhakikisha magonjwa hayo yanapata chanjo ili yatokee kabisa kama ilivyo kwa chanjo ya mdondo wa kuku ambayo imeleta mafanikio kwa kudhibiti ugonjwa huo nchini kwa asilimia 95 kwa wafugaji.

Meneja wa Taasisi ya Chanjo Tanzania, Dk Stella Bitanyi alisema kinazalisha dozi milioni 60 kwa mwaka kulingana na mahitaji, ingawa wanaweza kuongeza hadi kufikia milioni 100.

Dk Bitanyi alisema endapo watapatiwa vifaa zaidi wataweza kuzalisha zaidi na hata kuuza nje chanjo kwani chanjo zao zina ubora wa juu kiasi kuwa katika maeneo ya mipakani imegundulika chanjo ya mdondo inavushwa nchi za jirani za Malawi, Burundi na Kenya.

Katibu Mkuu Mifugo, Profesa Ole Gabriel alisema uzalishaji wa chanjo hapo nchini una faida tatu kubwa.

Alizitaja kuwa ni usalama wa nchi hasa kutokana na kuwapo kwa uhusiano mkubwa kati ya afya ya binadamu na ya mifugo, usalama wa afya ya watu na usalama wa afya ya mifugo.

Aliwataka wafugaji kutumia chanjo zinazozalishwa na TVI kwani zina ubora na zinapatikana kwa gharama nafuu.

Tanzania ni nchi ya pili kwa mifugo mingi barani Afrika baada ya Ethiopia, ikiwa na ng’ombe milioni 33.4, mbuzi milioni 21.9, kondoo milioni 5.7, kuku milioni 83.3, nguruwe milioni 2.2 na punda 660,000.

Sekta ya mifugo inakua kwa asilimia saba na inachangia Pato la Taifa kwa asilimia 7.6. Mwaka 2016 mapato ya sekta ya mifugo yalikuwa Sh bilioni 14.1, lakini mwaka huu yamefikia Sh bilioni 44.8 sawa na ongezeko la asilimia 210.

Chanzo: HabariLeo