0

Tanzania yajiandaa kuanza kuvuna helium

Tanzania yajiandaa kuanza kuvuna helium

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

TUME ya Madini imesema inasubiri Kampuni ya Helium One ya Norway iombe leseni ya uchimbaji wa gesi ya helium Ziwa Rukwa ili shughuli za uchimbaji zianze.

Kampuni ya Helium One ilikuwa ikifanya utafiti wa gesi hiyo katika Ziwa Rukwa na kubaini kuwepo kwa kiwango kikubwa cha gesi hiyo ambayo ni muhimu kwa uchumi wa Taifa na dunia.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya alilieleza HabariLEO jana kwa njia ya simu kwamba baada ya utafiti kukamilika, anayetakiwa kuthibitisha ni lini hasa uchimbaji wa gesi hiyo utaanza ni kampuni husika yaani Helium One kutegemea na uwezo wa kifedha na mtaji.

Profesa Manya alisema mpaka sasa kampuni hiyo haijaomba leseni ya uchimbaji wa gesi hiyo na itakapofanya hivyo, watatoa taarifa kwa umma.

“Baada ya kumaliza utafiti, watahitaji kuomba leseni ya uchimbaji ambayo bado hawajaomba, kwa hiyo kuhusu uchimbaji kuanza inategemea hela na mtaji wa kampuni husika, pia wenye uwezo wa kutangaza kiasi cha gesi kilichopatikana ni watafiti wenyewe,” alifafanua Profesa Manya.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema mpaka sasa Tanzania ni ya pili duniani kuwa na kiwango kikubwa cha gesi ya helium ikitanguliwa na Qatar ambayo tayari ilishaanza kuchimba gesi hiyo.

Akifungua Bunge la 12 jijini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais John Magufuli alilieleza taifa kuwa Tanzania ina tani nyingi za gesi ya helium Ziwa Rukwa na ikichimbwa inaweza kusambazwa dunia nzima kwa miaka 20.

Rais Magufuli aliwakumbusha Watanzania kuwa anaposema kuwa Tanzania si maskini ni kutokana na kuwa na rasilimali muhimu kama hizo.

Matumizi ya helium

Profesa Msanjila na Profesa Manya walisema gesi ya helium inatumika kwa mambo mbalimbali, lakini miongoni mwa matumizi makubwa ya gesi hiyo ni kutengenezea vitu vya kuzalisha baridi.

Matumizi mengine ni kutengeneza vifaa vya hospitali vya sumaku ikiwemo mashine ya kupima mwili ya MRI, nyaya za televisheni na intaneti zenye kasi kubwa, chip za kompyuta na simu, hadubini na pia hutumika kwenye ndege.

Kwa mujibu wa tovuti ya Helium One (http://www.helium-one.com/helium-market/), watumiaji wakubwa wa gesi ya helium ni katika sekta za afya, anga na elektroniki.

Alichokisema mtaalamu wa helium

Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ernest Mulaya amesema alifarijika baada ya Rais Magufuli kuwaonesha Watanzania utajiri wa gesi hiyo nchini unaokaribia kufikia futi za ujazo bilioni 138 kwa eneo la Rukwa tu.

Alisema kiasi hicho ni kikubwa na endapo nchi itaizalisha maana yake Tanzania ina uwezo wa kumsambazia kila mtu duniani ambako kuna jumla ya watu bilioni 7.8 kiasi cha mtungi wa futi za ujazo 18 zaidi ya lita 500.

“Habari njema ni kwamba gesi hii ya helium ni gesi ambayo kwanza baadhi ya matumizi yake hayana mbadala katika maisha na afya ya binadam hasa hospitalini mbali na matumizi mengine kama vile anga, vifaa vya electroniki, maabara na nyinginezo,” alisema Mulaya ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Durham nchini Uingereza.

Mulaya ambaye pia ni mwanachama wa kundi la utafiti wa gesi helium ya vyuo vya Durham na Oxford, Uingereza ambavyo vilishiriki katika uvumbuzi wa gesi hiyo mkoani Rukwa mwaka 2015, alisema hazina iliyopo ya gesi hiyo kwa sasa duniani imepungua lakini mahitaji ni makubwa yanayozidi upatikanaji hivyo kusababisha bei ipande.

“Kwa Tanzania gesi hii kwa mara ya kwanza ilivumbuliwa kabla ya uhuru katika miaka ya 1950 na Taasisi ya Utafiti Jiolojia ya Tanganyika hasa maeneo ya ziwa Balangida, ziwa Manyara na eneo la Majimoto na Mananka mkoani Mara,” alisema mtaalamu huyo wa jiolojia na jiosayansi ya gesi helium.

Alimshukuru Rais Magufuli kwa ushindi mkubwa katika sekta ya madini katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi vivyo hivyo katika gesi hiyo ya helium, lakini ni muhimu kuwa na mfumo mzuri na sera na mwongozo mahususi kwa ajili ya gesi hiyo adimu kabla ya kuingia katika makubaliano yoyote na kampuni za kigeni.

Pia alisema ni muhimu kuwekeza katika tafiti za gesi hiyo ili sera na mwongozo viendane na tafiti za kisayansi na akaishauri serikali iendelee kuhamasisha na kuwezesha wazawa kushiriki shughuli za utafiti, utafutaji hadi uzalishaji.

“Kwa kufanya hivyo tutawezesha utaalamu na ujuzi kubaki nchini kwa kiasi kikubwa na kujenga uwezo wa kisayansi kwa Watanzania walio wengi,” alisema.

Aliongeza: “Uzoefu umeonesha mara nyingi makampuni mengi hasa ya kigeni, hufanya utafiti na kuchukua data katika nci za Kiafrika lakini inapokuja utafsiri na uchakataji wa data hizo hufanyika nje ya nchi hivyo kuwanyima wazawa fursa ya kufanya kazi hizo ambazo ndio msingi wa kisayansi na uhakiki wa majibu ya rasilimali tulizonazo.

Chanzo: HabariLeo