0

Tanzania mshindi wa tatu tuzo za biashara duniani

Tanzania mshindi wa tatu tuzo za biashara duniani

Fri, 16 Oct 2020 Source: HabariLeo

TANZANIA imekuwa Mshindi wa Tatu kupata Tuzo za Taasisi zinazosimamia Biashara Duniani (WTPO 2020) katika kipengele cha matumizi bora ya ushirikiano katika huduma ya kliniki ya biashara inayosimamiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).

Tuzo hizo zimetangazwa juzi jijini Geneva, Uswisi ambapo Tanzania imewakilishwa na Balozi Maimuna Tarishi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika ofisi za Umoja wa Mataifa.

Tuzo hizo zinazosimamiwa na kutolewa na Kituo cha Biashara cha Kimataifa Duniani (ITC) ili kutambua michango ya taasisi zinazosimamia sekta ya biashara duniani (TPO) katika kusaidia wafanyabiashara wadogo na kati kuimarisha uzalishaji bora wa bidhaa zao, kuwajengea uwezo wa kufanya biashara na kuweza kuuza bidhaa wanazozalisha nje ya nchi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Theresa Chilambo, kwa mara ya kwanza Tanzania kupitia TanTrade imeweza kushiriki tuzo hizo katika kipengele cha matumizi bora ya ushirikiano kupitia huduma ya Kliniki ya Biashara kwa ushirikiano wa Benki ya Biashara ya Tanzania (NBC).

Huduma hii inalenga kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa nchini baada ya serikali kuwa na andiko la Blue Print ili kujenga mazingira rafiki ya ufanyaji biashara na kuweza kufikia uchumi wa viwanda.

Tangu kuanzishwa kwake, huduma hii imepokea changamoto za wafanyabiashara 1,083 na kufanikiwa kutatua changamoto 229 na kero 705 zinashughulikiwa.

Huduma imeweza kutolewa kwenye Maonesho 17 yaliyoratibiwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar, Pwani, Geita, Singida, Simiyu na Arusha.

Mashindano ya tuzo hizo hutolewa kila baada ya miaka miwili ambapo Tanzania kwa mara ya kwanza amekuwa mshindi wa tatu akitanguliwa na Uswisi na Vietnam katika kipengele cha matumizi bora ya ushirikiano.

Nchi nyingine zilizoshiirki katika kundi hilo ni Colombia, Misri, Uholanzi na Zimbabwe ambazo ziliingia kwenye kwenye mchujo wa mwisho

Chanzo: HabariLeo