0

TRA yaonya wanaodanganya makadirio ya kodi

TRA yaonya wanaodanganya makadirio ya kodi

Fri, 13 Nov 2020 Source: HabariLeo

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Manyara, imewaonya baadhi ya wafanyabiashara wanaotoa taarifa za uongo ili wakadiriwe kodi kidogo.

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Manyara, Eva Raphael alitoa onyo hilo mjini Babati wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Raphael alisema wafanyabiashara watakaobainika kufanya udanganyifu kwa kuwasilisha taarifa zao za udanganyifu ili wakadiriwe kiasi kidogo cha kodi, watachukuliwa hatua za kisheria.

Alisema wafanyabiashara wote wanapaswa kuwa waaminifu na wanaozingatia kutofanya udanganyifu katika ulipaji wa kodi.

Alisema kitendo cha kupeleka taarifa zao za udanganyifu katika uwasilishaji wa mapato ili kukadiriwa kodi ambayo siyo sahihi ni kosa.

"Waepuke udanganyifu kwa kuwa waaminifu katika ulipaji wa kodi ambayo mwisho wa siku inarudi kufanya maendeleo kwenye miradi mbalimbali ya wananchi," alisema.

Aliwataka wafanyabiashara kuzingatia matumizi sahihi ya mashine za EFDs na kutoa risiti wanapouza bidhaa zao.

Baadhi ya wafanyabiashara wa mjini Babati, akiwemo Josephine Joseph, walisema wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria ili kuepuka kuingia katika mikono ya sheria.

Lucas Samweli alisema wameshapatiwa na TRA elimu ya mlipa kodi, hivyo watatimiza hayo. Alisisitiza kuwa kitendo cha kuandikishia taarifa za uongo za mapato, kiepukwe kwani humwathiri vibaya mfanyabaishara husika ikiwemo kuchukuliwa hatua.

Chanzo: HabariLeo