0

TRA kuimarisha uadilifu kuongeza mapato

TRA kuimarisha uadilifu kuongeza mapato

Tue, 13 Oct 2020 Source: HabariLeo

NAIBU Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Msafiri Mbibo amesema mamlaka imejipanga kuimarisha uadilifu katika utendaji kazi ili kuongeza ukusanyaji mapato.

Akifungua mafunzo ya siku tatu kwa makatibu wa kamati za kudhibiti uadilifu katika mamlaka hiyo, Mbibo alisema kuimarika kwa kamati za kudhibiti uadilifu kutaiwezesha mamlaka hiyo kuwa taasisi yenye uadilifu na yenye kuendesha kazi vizuri kwa misingi ya haki ili kuongeza ukusanyaji mapato.

“Kama mnavyofahamu Tanzania imeingia uchumi wa kati ili tuweze kuhakikisha tunadumu katika uchumi wa kati au tunaenda zaidi ya tulipo ni lazima jamii yetu iendeshe mambo yake kwa uadilifu mkubwa na taasisi kama TRA ambayo ni nyeti ni lazima tuboreshe eneo la maadili,” alisema Mbibo.

Alisema TRA itahakikisha maadili yanazingatiwa katika utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa jamii ya Watanzania kwa kuzingatia misingi ya maadili ambayo ni uwajibikaji, uadilifu, na weledi.

Mbibo alisema TRA ina jukumu la kukusanya kodi kwa niaba ya serikali, na kwamba jukumu hilo haliwezi kutekelezwa kwa ufanisi bila kuwa na watumishi waadilifu na mfumo imara unaosimamia uadilifu

“Jukumu la TRA ni kukusanya kodi ambazo zinahusisha fedha, na fedha zina ushawishi lakini hata wateja wetu ambao ndio walipakodi wanaweza kuwa na ushawishi hivyo kupunguza fedha za serikali. Tukiimarisha uadilifu tutaongeza mwanamko wa wananchi kulipa kodi kwa hiari,” alifafanua.

Aliwaagiza makatibu kutekeleza majukumu kwa ufanisi ili kubadili taswira ya TRA mbele ya jamii kwa kuondokana na vitendo vya rushwa kwa watumishi na hatimaye kuongeza mapato ya serikali.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Ndani ya TRA, Amiram Lekey alisema mamlaka imeunda kamati hizo ili kutekeleza Mpango Mkakati wa Kupambana na Rushwa Awamu ya Tatu ulioanza mwaka 2017 hadi 2022.

“Lengo la mkakati huo ni kupunguza rushwa kwa kutumia mbinu za kuzuia na kupambana na rushwa hasa katika sekta zenye vishawishi vya rushwa ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania,” alisema Lekey.

Chanzo: HabariLeo