0

TIC mguu sawa kushughulikia uwekezaji

TIC mguu sawa kushughulikia uwekezaji

Mon, 12 Oct 2020 Source: HabariLeo

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) Dk Maduhu Kazi amesema kituo chake kimejipanga vema katika kuhakikisha kinaongeza ufanisi kushughulikia masuala ya uwekezaji, ili waweze kuwafikia wawekezaji wa ngazi zote.

Dk Maduhu alisema hayo jana wakati wa makabidhiano ya Chuo cha Ufundi (VETA), Kasoli kilichojengwa na mwekezaji Allience Ginnery Limited yaliyofanyika wilayani Bariadi.

Alisema kuwa kama ambavyo Rais John Magufuli amekuwa akisisitiza umuhimu wa uwekezaji endelevu nchini ,kituo chao hakina budi kuonesha juhudi na jitihada za dhati katika kuhakikisha wanaongeza ufanisi wa kuwahudumia na kutatua kero za wawezezaji wote bila kujali madaraja ya wawekezaji hao.

"Tumeahidi kufanya kazi na wawekezaji wote kwa kuwapa utaratibu, miongozo na kuwasaidia kutatua kero wanazokutana nazo katika uwekezaji wao...,"alisema.

Aliongeza kuwa wao kwa kushirikiana na serikali na mikoa husika wamekuwa wakiwalea wawekezaji hao vizuri na ndio sababu wengi wao wamekuwa wakirudisha faida waipatayo kwa jamii.

Aidha Dk Maduhu ameipongeza na kuishukuru Kampuni ya Alliance Ginnery kwa kujenga chuo cha ufundi ambacho kitakuwa na msaada mkubwa kwa wananchi waishio mikoa ya Simiyu na Mwanza, huku akiwataka wawekezaji wengine kuona umuhimu wa kuwafikia wananchi walio katika maeneo yao.

Naye Meneja mkuu wa kampuni ya Alliance Ginnery, Boaz Ogola wakati akikabidhi chuo hicho kwa mkurugenzi wa TIC, alisema kampuni yake imekuwa ikijihusisha na maendeleo ya jamii katika sekta ya afya, elimu, maji kwa kuwa ni wajibu wao kufanya hivyo na ni sehemu ya maelekezo kutoka kituo cha uwekezaji.

Aliongeza kuwa mpaka sasa kampuni yake imejenga majengo ya chuo cha ufundi kwa gharama ya Sh milioni 180, imechimba kisima kikubwa cha maji chenye uwezo wa kutoa lita 5,000 za maji kwa saa pamoja na kuweka vyerehani, majiko ya gesi na vifaa mbalimbali vya kujifunzia upishi na uashi.

Chanzo: HabariLeo