0

TBS yawataka wazalishaji nchini kuzingatia viwango

TBS yawataka wazalishaji nchini kuzingatia viwango

Mon, 9 Nov 2020 Source: HabariLeo

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wazalishaji waliopatiwa leseni na vyeti vya ubora kuwa mabalozi wazuri katika kuzingatia viwango ili kufikia lengo la Tanzania ya viwanda hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania ipo katika uchumi wa kati.

Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Yusuf Ngenya kwenye hafla ya utoaji vyeti na leseni kwa wazalishaji ambao bidhaa zao zimekidhi matakwa ya viwango.

"Muendelee kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango kwa mustakabali wa afya na mazingira ya watumiaji kwa ujumla," alisema.

Alisema leseni na vyeti vilivyotolewa mwishoni mwa wiki vitazisaidia bidhaa zilizothibitishwa kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kushindana sokoni na kuondoa usumbufu wa kupima bidhaa kwa kuzingatia matakwa ya mnunuzi.

Aidha, alisema vyeti na leseni hizo zitasaidia mzalishaji dhidi ya ushindani na bidhaa duni hafifu zisizo na ubora, kuongeza imani kwa umma juu ya ubora wa bidhaa iliyothibitishwa hivyo kupata wateja zaidi.

"Vyeti na leseni hizi zitawawezesha wazalishaji kuingia na kuuza katika soko la Afrika Mashariki pasipo kufanyiwa vipimo zaidi," alisema.

Kwa upande wa mlaji na watumiaji, Dk Ngenya alisema vyeti na leseni hizo zinawathibitishia kuwa bidhaa husika inafaa kwa matumizi ya binadamu.

"Inamhakikishia usalama wake kiafya na pia kulinda mazingira," alisema.

Kwa mujibu wa Dk Ngenya, wafanyabiashara hao wamepatiwa vyeti hivyo baada ya bidhaa zao kuthibitishwa ubora baada ya kukidhi matakwa ya viwango kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu, ambapo vyeti na leseni zilizotolewa ni 177.

Alisema kati ya leseni hizo, moja ni ya mfumo wa usimamizi ubora, 146 za alama ya ubora na 30 ni vyeti kwa bidhaa zisizo na viwango vya Tanzania.

Aidha, alisema kati ya leseni na vyeti vilivyotolewa, 88 ni vya wajasiriamali wadogo.

"Vyeti na leseni hizo ni za bidhaa za vyakula, vipodozi, vifaa vya ujenzi, vilainishi, vitakasa mikono, vifaa vya umeme, vifaa vya makenika, magodoro, vibebeo pamoja na vifungashio.”

"Naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa kuwahudumia wajasiriamali wadogo kupitia huduma za TBS juu ya uthibiti ubora bila malipo ya gharama za ukaguzi na upimaji.”

“Wajasiriamali wadogo hawa wataendelea kuhudumiwa bure kwa kipindi cha miaka mitatu ya mwanzo na baada ya miaka hiyo kuisha TBS itafanya tathmini ya uwezo wa wajasiriamali ili kupima uwezo wao wa kulipa," alisema.

Aliwataka wajasiriamali kuhifadhi vizuri kumbukumbu za uzalishaji na mauzo ili zisaidie katika kufanya tathmini.

Chanzo: HabariLeo